ALAT yasifu miradi ya afya Iringa
MAMLAKA ya Serikali za Mitaa nchini (ALAT) imetembelea baadhi ya miradi ya afya na elimu iliyojengwa mjini Iringa kwa ufadhili wa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC) Salim Asas na kusema watanzania wakiamua wana uwezo wa kiwango kikubwa wa kulijenga taifa wenyewe.
Baadhi ya miradi iliyojengwa au kukarabatiwa na Asas na kutembelewa na uongozi wa mamlaka hiyo ni pamoja na Ofisi ya Meya, jengo la maendeleo ya jamii, ofisi ya ardhi, soko la machinga na miradi kadhaa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa.
Mbali na michango yake mikubwa katika sekta hizo, asasi pia ni mdau mkubwa wa shughuli mbalimbali za maendeleo katika sekta nyingine, jamii, siasa na watu wenye uhitaji wa ziada.
Akitoa pongezi kwa MNEC huyo mara baada ya kutembelea baadhi ya miradi aliyoifadhili mjini Iringa, Makamu Mwenyekiti wa ALAT Taifa, Sima Constantine Sima alisema ziara yao ililenga kukagua ushiriki wa wadau wa maendeleo katika kuunga mkono juhudi za serikali za kuboresha maisha ya wananchi.
Katika kutambua mchango wake mkubwa katika shughuli hizo, ALAT ilimtunuku Asas cheti cha pongezi kama ushahidi unaothibitisha mamlaka hiyo jinsi inavyotambua mchango wake kwa maendeleo ya ndani na nje ya mkoa wa Iringa.
“Mamlaka na serikali kwa ujumla inautambua na kuuthamini mchango wako katika kusukuma gurudumu la maendeleo ya Taifa.
Michango mingi unayotoa inagusa mahitaji ya moja kwa moja ya wananchi hatua inayoipunguzia serikali gharama,” alisema na kuwataka wadau wengine kuiga.
Akielezea ukubwa wa michango ya Asas katika manispaa yake, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa Ibrahim Ngwada alisema haielezeki kirahisi kwani kila mahali palipohitaji mchango wake amefanya kwa uwezo wake.
Akiwaomba wadau wengine kuunga mkono kile kinachofanywa na Asas, Ngwada alisema maendeleo ya mji huo yanahitaji mchango wa wadau wake wote na dhana hiyo ikiwepo Iringa itakuwa kwa kasi zaidi.
Alisema sekta ya afya ni moja ya eneo nyeti ambalo kwa mchango wa Asas limeboreshwa kuwezesha baadhi ya huduma zilizokuwa hazitolewi, kuanza kutolewa.
“Katika hospitali yetu ya mkoa, tumejengewa wodi ya wagonjwa wa daraja la kwanza yaani VIP, jengo la ICU, jengo la viungo bandia na jengo la watoto njiti,” alisema na kutaja michango mingine mingi katika sekta hiyo, elimu, miundombinu na biashara.
Akitoa mfano wa tukio la hivikaribuni Mstahiki Meya alisema Asas amesaidia kuboresha miundombinu ya Soko la Machinga katika eneo la makaburi ya Mlandege baada ya kutoa milioni 100 kwa ajili ya kazi hiyo.
Alisema kitendo cha ALAT kushukuru na kutambua mchango mkubwa unaofanywa na wadau ni cha kupongezwa kwani kinawatia moyo wadau hao kuendelea kujitoa zaidi katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
Kwa upande wake Asas ameishukuru ALAT kwa kutembelea mkoa wa Iringa na kutambua mchango wake katika kuharakisha maendeleo ya mkoa na Taifa kwa ujumla.
Alisema anasukumwa kuchangia maendeleo akiamini kutoa ni moyo na wala si utajiri na kwamba hata watu wenye kipato kidogo wanaweza kuzishughulikia changamoto zao za kimaendeleo kama wakiunganisha nguvu kwa chochote walichonacho.
“Tukisema kila jambo lisubiri serikali tutachelewa maana serikali ina mambo mengi ya kufanya na inafanya kwa kuzingatia bajeti na mipango yake. Kwahiyo yale yanayoweza kuchangiwa na wadau wakiwemo wananchi basi ifanyike hivyo,” alisema.