‘Sina ubaya na viongozi Simba’

DAR ES SALAAM; MWANACHAMA wa klabu ya Simba SC, Agness Daniel ‘Aggy Simba’ amesema hajawahi kukosana na kiongozi yeyote wa klabu hiyo.

Akizungumza na HabariLEO, Aggy mapema hii leo, amesema kikatiba ni haki yake kuhoji anapoona baadhi ya mambo ya klabu hayako kwenye mstari.

Hatua hiyo imekuja baada ya Juni 15, 2024 sekretarieti ya klabu hiyo kuwasimamisha wanachama wawili Mohammed Khamis Mohammed na Agness Daniel mpaka pale kamati ya maadili itakapoamua vinginevyo.

HabariLEO ilimtafuta Aggy Simba kutaka kufahamu kuhusu kusimamishwa kwake na nini kitafuata baada ya hapo.


Akijibu swali hilo, Aggy amesema hafahamu sababu za kusimamishwa, hivyo anasubiri kuitwa kwenye kamati kuona itaamuaje.

“Nimeona barua kwenye mitandao ya kusimamishwa kwangu kwa sababu zilizotajwa na wao, pia barua imesema tutaitwa kamati ya maadili na mimi nasubiri kuitwa kwenye kamati ya maadili, ili nijue makosa yangu ni yapi kikatiba,” amesema Aggy Simba.

Alipoulizwa kama anatamani siku moja awe kiongozi wa Simba, amesema hafikirii hilo kwani anafurahia zaidi kuwa mwanachama.

Habari Zifananazo

Back to top button