Amani, utulivu, upendo viwe msingi wa Sikukuu ya Pasaka

DAR ES SALAAM; WAKRISTO nchini leo wanaungana na wenzao kote duniani kusherehekea Sikukuu ya Pasaka kukumbuka ufufuo wa Yesu Kristo miaka zaidi ya 2000 iliyopita.

Sikukuu hii ya kiimani ni kilele cha mfungo wa Kwaresima wa siku 40 walioufanya Wakristo kukumbuka mateso, kifo na ufufuo wa mwokozi wao, Yesu Kristo.

Katika kipindi chote cha Kwaresima, tumeshuhudia waumini wa Kikristo wakitekeleza msingi huo wa imani kwa kufunga, kusaidia wahitaji na kufanya ibada ambazo tunaamini zimewasogeza zaidi karibu na Mwenyezi Mungu.

Ni imani yetu kwamba, leo wanaposherehekea Pasaka, wataendeleza mema walioyafanya wakati wa Kwaresima na kuhakikisha imani inawajenga zaidi kuwa raia wema kwa nchi yao Tanzania.

Tunatumaini sherehe hii yenye maana kubwa katika imani ya Kikristo itaongeza hari ya watu kufanya kazi kwa bidii katika maeneo yao ya kazi, biashara na uwekezaji lakini pia itachagiza upendo, amani na utulivu hasa tunapoelekea katika Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu.

Tunategemea wazazi waendeleze malezi bora na mema kwa watoto, wakihakikisha katika sherehe hii wanafurahi na kupatiwa ulinzi kuanzia ngazi ya familia, mtaani na jamii kwa ujumla.

Hatutarajii kuona watoto wanazagaa hovyo mitaani bila uangalizi wa watu wazima. Hatutegemei kuona watoto wakiachwa peke yao majumbani bila uangalizi kwa kuwa hata nyumbani zipo hatari zinazoweza kutokea msimu huu wa sikukuu.

Jeshi la Polisi katika maeneo mbalimbali nchini limeeleza limejipanga ipasavyo kuhakikisha Pasaka inakuwa ya amani na utulivu. Jukumu hili si la Polisi peke yake bali ni la jamii nzima.

Tunashauri watu wasikae kimya watakapoona kuna viashiria vya uvunjifu wa amani katika sherehe hii na kwa wale wanaotumia vyombo vya moto, wahakikishe wanazingatia sheria na kanuni za usalama barabarani.

Tunawakumbusha madereva kuepuka kuendesha vyombo vya moto kwa mwendo kasi, kuepuka kutumia vilevi kupindukia na kuendesha kwani kufanya hivyo ni kinyume cha sheria lakini pia, ni sababu ya ajali za kizembe zinazoweza kuzuilika.

Tunaamini Sikukuu hii ya Pasaka itaendeleza amani, upendo na utulivu uliopo nchini na tunatarajia waumini kutekeleza yale yatakayoelekezwa na viongozi wao katika nyumba za ibada leo ili Tanzania iendelee kuwa mahali salama na pazuri pa kuishi.

HabariLEO tunawatakia Wakristo wote nchini heri ya Pasaka!

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button