MAREKANI: SHIRIKA la Haki za Binadamu la Amnesty International limesema pande zote mbili zinazohusika na vita nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) huenda zimekiuka sheria za kimataifa za vita kwa kushambulia maeneo yenye msongamano wa raia.
Taarifa iliyotolewa na Amnesty International Jumatatu, inasema zaidi ya raia 100 waliuawa mashariki mwa Congo mwaka 2024.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa Jeshi la Congo pamoja na waasi wa M23 wanahusika na ongezeko la matumizi ya silaha zisizo sahihi, huku raia wakikosa ulinzi.
Kundi la M23, linalodai kuwa linawalinda Watutsi, lilirejea tena mwishoni mwa mwaka 2021 kwa msaada wa wapiganaji kutoka Rwanda, na limefanikiwa kuteka maeneo mengi ya Mashariki mwa Congo, eneo lenye utajiri wa madini.
Hali hiyo imezusha mgogoro mkubwa wa haki za binadamu, na kusababisha maelfu ya watu kuyakimbia makazi yao. SOMA : DR CONGO : ADF yaua watu 12 Congo
Shirika la Amnesty International limeongeza kuwa mashambulizi haya yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 100 na majeraha kwa wengine, huku pande zinazohusika zikiendelea kukiuka sheria za kimataifa zinazohusiana na ulinzi wa raia katika kipindi cha vita.