Andengenye afichua mbadala wa ajira wahitimu JKT
KASULU, Kigoma: MKUU wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye amewataka vijana waliohitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kutumia ujuzi waliopata kujiajiri kwakuwa Tanzania hakuna changamoto ya kazi ingawa kuna changamoto ya ajira.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya awali ya kijeshi ya vijana wa kujitolea Operesheni miaka 60 ya JKT katika kikosi cha Jeshi 825 Mtabila iliyopo wilayani Kasulu Mkoa wa Kigoma, Mkuu wa Mkoa huyo amesema kupitia mafunzo hayo jeshi linajivunia kuwa na jeshi la akiba imara na hodari na matunda ya kazi hiyo ni kuona taifa linaendelea kuwa na amani na utulivu na kuwa viongozi wenye kulipenda taifa na ndio msingi wa kiapo chao.
“Mafunzo mliyoyapata nendeni mkayatumie vizuri ili kutimiza lengo kuwaanda jeshi la akiba na kamwe msikubali mtu yeyote awalaghai na mkajiunga na vikundi vya uhalifu kwani huo utakuwa ni usaliti wa kiapo chenu na usaliti kwa taifa,” amesema Andengenye.
Kiongozi huyo pia amewaasa wahitimu hao kutokubali kulaghaiwa na kujiunga na vikundi mbalimbali vya kihalifu, kwani kukubali kulaghaiwa ni usaliti wa kiapo cha jeshi na usali kwa taifa ambalo limetumia gharama kubwa kuwaandaa.
Kwa upande wake Muwakilishi wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Mkuu wa Tawi la Ugavi, Uchukuzi na Uhandisi Makao Makuu ya Jeshi, Meja Jenerali Hawa Kodi amewataka vijana hao kutumia jukwaa hilo kuwaelimisha wengine kwa vitendo kuwa wao ni wazalendo na kujiepusha vitendo vitakavyowaingiza kwenye matatizo ya afya ya mwili na afya akili.
Naye, Muwakilishi wa Mkuu wa JKT, Mkuu wa Tawi la Utawala JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena amesema kufuatia mafunzo hayo vijana hao watakuwa tayari kutumikia na kulilinda taifa popote watakapokuwa na kuwataka kutumia elimu waliyoipata katika kutatua changamoto mbalimbali pasipo kuvunja sheria, kanuni na taratibu za nchi.