‘Anzisheni viwanda mazao ya mifugo Katavi’

Serikali mkoani Katavi imetoa wito kwa wawekezaji wa ndani na nje wa mkoa huo kufungua viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo, ambavyo vitachangia ukuaji wa uchumi pamoja na kuimarisha lishe kwa wananchi.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko wakati alipokuwa akikabidhi vifaa vya uchakataji wa mazao ya mifugo na vifaa vya kuhifadhia mifugo vilivyotolewa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa Chama cha Ushirika cha Maziwa cha Kashaulili wilayani Mpanda.

Amebainisha kuwa Mkoa wa Katavi kutokana na Sensa ya mifugo ya mwaka 2022, ulibainika kuwa na jumla ya mifugo zaidi ya 800,000, hivyo mkoa huo kuwa na mifugo ya kutosha hadi kufanya uhitaji wa viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo, na kutokana kuongezeka kwa kasi kubwa ya mifugo kwa sasa Mkoa unakisiwa kuwa na mifugo zaidi ya milioni moja.

Mrindoko amewataka wananchi wa Katavi na nje ya Mkoa huo kufungua viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo kwa kuwa wawekezaji si lazima wawe ni wageni kutoka nje ya nchi.

“Mkoa wa Katavi unahitaji zaidi viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo, kuanzia nyama, ngozi na maziwa hivyo chama hiki cha Ushirika wa maziwa cha Kashaulili muhakikishe mnaanzisha kiwanda cha kuchakata mazao ya mifugo,” amesema.

Ameongeza kuwa kutokana na hali hiyo Serikali ipo tayari kuendelea kuimarisha sekta ya mifugo kupitia mipango ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, hivyo wanahitaji viwanda vyingi kwenye mkoa huo.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Hassan Rugwa amesema kuwa, huo ni mwanzo mzuri ambao utawafanya watu wengine waweze kuvutika na kuanzisha viwanda vingine vya kuchakata mazao ya mifugo kwenye Mkoa huo kutokana na mahitaji yaliyopo.

Naye Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu ameahidi kwamba watafuatilia na kusimamia vifaa hivyo, ili kuhakikisha vifaa hivyo vinatumika na kuzalisha kwa tija.

Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika Kashaulili, Charles Ngonyani amesema kuwa vifaa hivyo walivyokabidhiwa na serikali vitawasaidia kuwa na uhakika wa kupata maziwa yenye ubora na yaliyo salama zaidi.

Habari Zifananazo

Back to top button