KATIKA kuweka jiji la Arusha katika hadhi ya kimataifa jiji hilo sasa litawekwa taa katika barabara zote na kufungwa CCTV Camera lengo ni kuliweka katika hali ya ulinzi na usalama.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Filician Mtehengerwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika kata ya Daraja Mbili jijini Arusha.
Mtehengerwa alisema jiji hilo linaitwa Geneva ya Afrika hivyo basi sifa hiyo inapaswa kwenda na uhalisia na kutokana na hali hiyo serikali imetenga zaidi ya Sh bilioni 1 kufunga taa katika barabara zote za jiji hilo.
Alisema mbali ya serikali kutenga fedha hio serikali imetenga fedha nyingine kwa ajili ya kufunga CCTV Camera katika mitaa yote ya jiji la Arusha ili wenye kufanya uhalifu waweze kuchukuliwa hatua haraka iwezekanavyo.
‘’Tunataka mama akisahau beki lake au akidondosha kalamu apelekewe na sio kuchukuliwa na vibaka sasa watafute kazi nyingine maana serikali imejipanga’’alisema Mtehengerwa
Aliwataka madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Arusha kuhakikisha wanapata mwekezaji mwenye vyombo vya kisasa vya kuzoa taka na kuchakata na sio mwekezaji wa kuzoa taka na kwenda kutupa katika dampo kwani stahili hiyo imepitwa na wakati kwa hadhi ya jijj.
Alisema haiwezekani kila kona majalala ya matakataka hilo sio sawa mwekezaji mwenye vyombo vya kisasa anapaswa kupewa kazi hiyo na ifike wakati madiwani wawajibike katika kumsaka mwekezaji huyo.
Mkuu huyo alisema jukumu hilo sasa liko mikononi mwa madiwani kushirikiana katika kumsaka mwekezaji mwenye sifa ikiwemo uwezo wa kuchakata takataka na kuzifanya kuwa mbolea kwa wakulima na jiji linapaswa kuendeshwa kisasa kulingana na hadhi yake.
‘’Jiji la Arusha ni Geneva ya Afrika hivyo basi jina hilo linapaswa kwenda na uhalisia wake kwa kuwa na taa katika barabara zote,kufungwa CCTV Camera katika kila kona na kuwa na magari ya kisasa ya kuchakata taka ‘’ alisema Mtehengerwa
Akizungumzia ulinzi alisema kata inayoongoza kwa uhalifu katika jiji la Arusha ni kata ya Daraja Mbili hivyo amewataka wazazi kuwaonya watoto wao vinginevyo wasimfuate kwa lolote litakalowatokea.
Mtehengerwa ametoa mwezi mmoja kuhakikisha zinapigwa kura ya kuwataja wahalifu wote wa kata hiyo kuchukuliwa hatua kwani kata ya Daraja Mbili inaongoza kwa uhalifu na serikali haiwezi kuliacha hilo.
Naye diwani wa kata hiyo,Prosper Msofe alimuomba Mkuu wa Wilaya kutoa ushirikiano na baadhi ya viongozi wa kata hiyo akiwemo mtendaji wa kata John Joseph kudhibiti wahalifu kwani kata hiyo ina vijana wenye sifa mbaya ya uhalifu.