Arusha mguu sawa UMISSETA Taifa

ARUSHA: MKOA wa Arusha umekamilisha maandaalizi yake kwa ajili ya mashindano ya kitaifa ya Umoja michezo kwa shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) yanayotarajiwa kuanza kuchezwa Juni 19 hadi 30 mwaka huu mkoani Iringa.
Jumla ya wachezaji 120 ambao ni wasichana na wavulana wamechaguliwa kuunda timu ya mkoa ya UMISSETA ambayo tayari iko kambini kwa ajili ya kujiweka imara zaidi kabla ya kuanza safari yake kuelekea mkoani Iringa.

Mchujo huo ulihusisha wilaya zote saba za mkoa wa Arusha ambazo zilishiriki katika kutoa wachezaji hao 120 waliounda timu ya mkoa katika michezo mbalimbali.
Michezo hiyo ni mpira wa miguu, wavu, kikapu, riadha, netiboli, mpira wa mkono, mpira wa goli, sanaa mbalimbali na michezo mingine.
Zoezi zima la kuhitimisha michezo hiyo kimkoa lilifanyika katika uwanja wa shule ya Ilboru uliopo Arusha DC.
Akizungumza katika hitimisho hilo mbele ya wanafunzi walioshiriki kutoka halmashauri saba, Ofisa Elimu Taaluma Mkoa wa Arusha Tumsifu Mushi ambaye alimuwakilisha Ofisa Elimu Mkoa ,amesema mashindano hayo ni chachu na yanawapa vijana hamasa kuonyesha vipaji.
“Michezo ina manufaa mengi hivyo nawasihi wanamichezo hawa waliopata nafasi ya kuunda timu ya mkoa waende kucheza kwa bidii ili vipaji vyao vionekane na wapate nafasi ya kusonga mbele kimichezo,” amesema.
Amewapongeza wote walioshiriki kikamilifu katika maandalizi ambayo yalianzia wilayani na hatimae kuhitimishwa mkoani.
Naye Ofisa Michezo,Utamaduni na sanaa wa Halmashauri ya Jiji la Arusha Lucy Jilanga amesema wamepata wachezaji 120 katika michezo yote itakayoshindaniwa pia fani za ndani ambao sasa wapo kambini kuendelea kujinoa zaidi hadi tarehe 18 Juni ambapo ndipo safari ya kuelekea Mkoa Iringa kushiriki kitaifa.
“Kwa msimu huu tunawaahidi ushindi mkubwa wana Arusha kwa sabbau watoto hawa wamejiandaa kuanzia shuleni na mchuano ulikuwa mkali na wale mahiri ndio wamechaguliwa hivyo Taifa likae kao wa kula kuwa tunakwenda kubeba vikombe vyote,”amesema Jilanga.
Kwa upande wake, Menard Meshack Lupenza ambaye ni Ofisa Elimu shule za Sekondari kutoka Arusha Dc, amewasihi wanafunzi hao waliochaguliwa kuzingatia nidhamu katika kipindi chote cha mashindano na kusema maafisa Elimu wote wako nao bega kwa bega kuona wanafanya vizuri na kuuletea mkoa Ushindi.



