TABORA – WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro ameagiza Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuhakikisha vyama vya michezo vinajumuisha kwenye timu za taifa wachezaji chini ya miaka 17 na 20 wanaotokana na michezo ya Umitashumta na Umisseta.
Pia alisema kuanzia mwaka 2024/25, serikali itajenga viwanja vya michezo na sanaa katika shule 10 ikiwa ni sehemu wa mpango wake wa kujenga viwanja hivyo kwa shule mbili kila mkoa.
Dk Ndumbaro alisema hayo jana mkoani Tabora wakati wa kufungua mashindano ya Umisseta yanayoendelea mkoani Tabora. Alisema BMT lazima isimamie na kuhakikisha vyama vya michezo vinajumuisha kwenye timu za taifa wanazoziunda wachezaji kutoka kwenye michezo ya Umisseta na Umitashumta.
“BMT simamieni hili, ili vyama vya michezo yote vinapounda timu zao za taifa lazima zijumuishe na wachezaji wanaotokana na mashindano haya angalau hata mmoja. Wa shule za msingi waende timu za chini ya umri wa miaka 17 na sekondari waende za chini ya umri wa miaka 20.”
SOMA: Ntibazonkiza Ntibazonkiza yametimia Simba
Aidha, Ndumbaro alisema serikali itajenga viwanja vya michezo katika shule mbili kwa kila mkoa na itaanza na shule 10 Tabora, Tanga, Dodoma, Manyara, Pwani, Singida, Ruvuma, Kagera na Mtwara.
Alisema Rais Samia Suluhu Hassan ameboresha mashindano hayo kwa kuongeza fedha mwaka kila mwaka na kuhakikisha yanafanyika kwa heshima na mafanikio makubwa.
Ndumbaro alisema kutokana na umuhimu wa michezo, wizara yake, Ofisi ya Rais -Tamisemi na ya Elimu zimekuja na falsafa ya michezo ni ajira na ni uchumi.