MFANYABIASHARA Harid Njianguru mkazi wa Kidatu Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro anasakwa na polisi kwa tuhuma za kumshambulia mteja wake na kusababishia madhara makubwa baada ya kushindwa kulipa kiingilio cha Sh 500 kuangalia mpira kati ya timu ya soka ya Azam FC na Tanzania Prisons kwenye ukumbi wa baa anayomiliki.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Alex Mkama alisema tukio hilo lilitokea usiku wa Agosti 28, 2023 katika kijiji cha Mkamba Wilaya ya Kilombero baada ya mfanyabiashara huyo kumshambulia Protas Komba (40) kwa kumpiga na kisha kumsukuma na kuangukia kisogo na kupoteza fahamu.
Alisema Komba alifika baa ya mfanyabiashara huyo ambayo inajulikana kwa jina la‘ Kigamboni’ ili kuangalia mchezo huo na kwamba alishindwa kulipa kiingilio cha sh 500 na akawa analazimisha kuingia ndani ya baa.
“Komba alipoingia ndani mwenye ukumbi huo hakutaka aagalie ule mpira akamzuia na akamsukuma na kumpiga kuangukia kisogo na akawa amepoteza fahamu na hivyo alikimbizwa hospitali “ alisema Kamanda Mkama.
Kamanda Mkama alimewaomba wananchi kuwa popote mtuhumiwa huyo atakapoonekana taarifa zake zitolewe ili aweze kukamatwa kwa sababu hawezi kuwa salama kwa namna yoyote ile.
Mkama alitoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake watumie njia zinazokubalika kisheria na kupata haki zao .
“ Michezo ni burudani na kama mtu anatafuta burudani basi ifanyike namna ya kuweza kufanya mazugumzo kama kuna ulazima ili na yeye aweze kushiriki kwenye burudani, kama haiwezekani basi atumie lugha za staha kuliko mkumzuia na kusababisha kitendo kilichofanyika kilicholeta madhara makubwa.” alisema Mkama
Kwa mujibu wa ratiba ya Bodi ya Ligi, NBC Premier League siku ya Agosti 28, 2023 ulifanyika mchezo mmoja kuanzia majira ya saa moja usiku kati ya timu ya Azam FC dhdi ya Tanzania Prisons ambapo Azam FC iliibuka na ushindi wa bao 3-1.