Asas aonyesha matumaini ya ushindi mkubwa wa CCM

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Salim Asas amepiga kura na kuonyesha matumaini kuwa viongozi watakaochaguliwa katika uchaguzi huu wa serikali za mitaa watakuwa na mchango mkubwa katika kusukuma maendeleo ya mkoa wa Iringa na taifa kwa ujumla.

Akizungumza mara baada ya kushiriki katika zoezi la upigaji kura kuchagua Mwenyekiti wake wa mtaa wa Chuo cha Afya, Asas aliwapongeza wananchi wa Iringa kwa kujitokeza kwa utulivu na kwa wingi, akisisitiza kuwa ushiriki wa kila mmoja ni muhimu katika kujenga msingi thabiti wa demokrasia.

“Nina imani kubwa kuwa uchaguzi huu utaibua viongozi wenye maono ya kweli ya maendeleo. Wananchi wanapaswa kuendelea kujitokeza kwa wingi na kutumia haki yao ya kidemokrasia kwa amani na utulivu, kwani maendeleo ya taifa letu yanategemea maamuzi tunayoyafanya leo,” amesema Asas.

Advertisement

Aliwakumbusha wananchi akisema uchaguzi ni fursa ya kipekee ya kuimarisha mustakabali wa taifa, hivyo ni muhimu kuendelea kushirikiana licha ya tofauti za kisiasa.

Asas alionyesha matumaini makubwa kuwa chama chake cha CCM kitapata ushindi mkubwa, akitaja juhudi kubwa zilizofanywa na chama hicho katika kuimarisha sekta za elimu, afya, na miundombinu kama msingi wa matumaini hayo.

Huku uchaguzi ukiendelea, viongozi wa dini na mashirika yasiyo ya kiserikali wameungana na wadau wengine kuhimiza amani, mshikamano, na kuheshimu matokeo ya uchaguzi.