Asas atuliza hofu Iringa: “Mimi ni yuleyule, cheo hakitanibadilisha”

IRINGA: Katika tukio lililobeba uzito wa kihistoria na hisia za kipekee za kisiasa, Salim Asas, mmoja wa viongozi wenye mvuto, ametikisa nyoyo za wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wananchi waliokusanyika kumpokea baada ya uteuzi wake kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (MCC).
Katika hotuba yake iliyogusa nafsi, Asas hakusita kuweka wazi mzigo alioubeba, dhamira yake na hofu ya Mungu mbele ya dhamana hiyo.
“Ningekuwa na uamuzi, nisingependa shughuli kama hii ifanyike. Hii si nafasi ya kusherehekea, ni nafasi nzito yenye wajibu mkubwa kwa chama na taifa. Ukikosea, unaharibu sura ya chama na aliyekupendekeza,” alisema kwa msisitizo wakati wana CCM wakimpokea na kumpongeza kwa kuteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa.

Asas, ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kupitia Mkoa wa Iringa (MNEC), alitumia jukwaa hilo kutoa shukrani kwa wanachama wa CCM mkoani Iringa kwa kumpa heshima ya kuwa miongoni mwa waliomuwezesha kufikia uteuzi huo.
“Bila nyinyi kunichagua kuwa MNEC, nisingekuwa hapa. Nawashukuru kwa moyo wangu wote, shukrani hizi ni zenu,” alieleza kwa hisia kali.
Kwa heshima ya nafasi hiyo, alitoa pongezi na shukrani za dhati kwa Rais, Dk Samia Suluhu Hassan, kwa kumpendekeza na kwa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) kuridhia uteuzi huo.

Kwa sauti ya kujiamini na kuonyesha msimamo wa chama chake, Asas alieleza kwamba ajenda yake ya kwanza ni kuhakikisha ushindi mkubwa kwa CCM na Rais Samia katika uchaguzi mkuu ujao.
“Nitaenda pori kwa pori, mtaa kwa mtaa, kuhakikisha Mama anapata kura za kutosha. Haiwezekani Mjumbe wa Kamati Kuu atoke Iringa halafu kura za mama ziwe za mashaka. Haiwezekani,” alisisitiza huku umati ukimshangilia.

Ajenda yake ya pili, ni kutekeleza kwa uadilifu wajibu wake kama mjumbe wa vikao mbalimbali vya chama.
“Nitakuwa sehemu ya vikao vinavyojadili wagombea, kuanzia mkoa hadi Taifa. Nitaomba hekima kwa Mwenyezi Mungu nitende haki. Naomba dua zenu, naomba ushirikiano wenu,” alisema.

Akiwa mtu wa vitendo, Asas alisema tayari ameanza kupitia Katiba ya CCM kipengele kwa kipengele, akisema nafasi hiyo aliyopewa inashtua mwili kwa jinsi inavyobeba majukumu mazito ya chama na nchi.
“Ukisoma Katiba ya chama chetu na majukumu ya Kamati Kuu, mwili unasisimka. Hii si nafasi ya kupendelewa, ni nafasi ya kufanya kazi kwa moyo safi kwa ajili ya chama na wananchi.” alisema.
Kwa maneno yaliojaa unyenyekevu na heshima kwa wananchi, Asas alihitimisha hotuba yake kwa kusema:
“Mimi ni Salim yule yule. Sitabadilika kwa sababu ya cheo. Nitaendelea kuwa miongoni mwenu mitaani na kwenye chama kama kawaida. Cheo ni dhamana – sitakitumia kwa faida yangu binafsi.”
Katika salamu mbalimbali za viongozi wa chama na serikali, maneno yalikuwa na mwelekeo mmoja: haki hii ameistahili kwa utumishi wake uliotukuka kwa chama, kwa mkoa na kwa Taifa.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba, alisisitiza kuwa uteuzi huo ni zawadi ya Rais Samia kwa Iringa kutokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayojionesha wazi.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Daudi Yasin, alimpongeza Asas akisema: “Zawadi ya kipekee tutakayompa Dk Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha anapata mitano mingine kwa kura nyingi mkoani Iringa na kata zote na majimbo yote tunabeba.”
Viongozi mbalimbali wa CCM na serikali – akiwemo Mstahiki Meya wa Manispaa, wabunge na mawaziri, madiwani, viongozi wa mashina, wasanii, bodaboda, bajaji, machinga na wazee wa kimila – walijitokeza kwa wingi na kutoa salamu za pongezi na kuahidi ushirikiano na mshikamano.
Kwa muktadha wa kisiasa, uteuzi wa Asas umegeuka kuwa mwamko mpya wa siasa Iringa na kwa wasiojua hadi mawaziri tunakuwa chini ya uongozi wake, alisema Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Jumuiya ya Afrika Mashariki Cosato Chumi.
“Ni kama mwamvuli mpya unaofunika matumaini ya wananchi kuelekea uchaguzi mkuu, una historia kubwa ya kukipenda chama, unajitoa kutumia muda na rasilimali zako kukitumikia chama na tena kwa misingi ya haki,” alisema Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile.
Naye Mbunge wa Kalenga Jackson Kiswaga na Kilolo Justine Nyamoga walisema kwa Salim Asas, jina lake sasa limeunganishwa moja kwa moja na hatima ya ushindi wa chama kwa ngazi zote.
Mbunge wa Viti Maalumu, Rose Tweve alisema kilichomfikisha Asas katika nafasi ya juu ya chama hicho ni nidhamu na utii kwa chama chake.
“Na sisi wengine tujifunze: ukitenda mema, Mungu atalipa,” alihitimisha Mbunge wa Iringa Mjini, Jesca Msambatavangu.
Katika hali iliyogusa nyoyo, viongozi wa dini waliomba kwa ajili yake — aepushwe na husuda, wakisema “Hili ni chaguo la Mungu.”
Huku viongozi wa kimila wakimsimika na kumpa jina la Mwendavanu — wakimaanisha mpenda watu.
“Kwa sasa, si Iringa tu inayomwangalia Asas kwa matumaini, bali taifa linamwona kama kiongozi mpya wa kutegemewa katika kuimarisha umoja wa CCM na kusimama imara katika maamuzi ya chama na mustakabali wa nchi,” alisema Chifu Adam Abdul Sapi Mkwawa.

