Asas: Vijana wamtetee Rais Samia

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Salim Asas, amewasihi vijana wa chama hicho wasitumie mitandao ya kijamii kwa kuonesha tu maisha yao binafsi, bali watumie majukwaa hayo kuwajibu vikali wanaomchafua Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa tuhuma za uongo.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo maalumu ya vijana wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Iringa yaliyofanyika kwa siku saba katika Chuo cha Ihemi, Iringa Vijijini Asas aliwakosoa baadhi ya vijana ambao, badala ya kutumia mitandao kulinda viongozi wao, wamekuwa:

“Wakijikita katika kujionyesha wakiwa na marafiki zao au kuonyesha umaridadi wao bila kujali mashambulizi wanayopata viongozi wa serikali na chama, hususan Rais.

“Asilimia 70 ya hotuba za wapinzani zinajikita kumshambulia Rais Samia kwenye mitandao ya kijamii. Inasikitisha kuwaona vijana wetu wakiwa kimya bila kutoa majibu. Ni lazima vijana wasimame imara na kujibu mapigo,” alisema Asas.

Ameongeza kuwa ni jukumu la vijana wa UVCCM kuhakikisha kuwa wanajibu propaganda za wapinzani na kuweka bayana mafanikio ya serikali ya awamu ya sita kwa kuonesha kazi nzuri zinazofanywa na serikali, katika sekta za afya, miundombinu, maji, elimu na nyinginezo.

Asas amesisitiza kuwa vijana hao wanatakiwa kutumia angalau asilimia 70 ya muda wao mtandaoni kumtetea Rais na serikali, badala ya kuruhusu wapinzani kueneza uongo bila kupingwa.

“Tusiwe baridi. Tukimtetea Rais Samia na viongozi wengine, tunawapa moyo wa kuendelea kuchapa kazi. Hivyo, ni muhimu vijana kusimama imara mitandaoni na kueleza kwa vitendo mafanikio makubwa yanayoendelea kufanyika nchini,” alisisitiza.

Vijana hao wa UVCCM walionyesha mwamko mkubwa, wakiahidi kutumia nguvu zao zote kulinda hadhi ya chama na viongozi wake.

Wamesema wako tayari kumtetea Rais Samia na serikali yake dhidi ya tuhuma za wapinzani, huku wakijiandaa kikamilifu kwa chaguzi zijazo, ikiwemo uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwakani.

Katibu wa UVCCM Mkoa wa Iringa, Aisha Mpuya, amesema mafunzo hayo yalilenga kuwaongezea vijana uelewa wa matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii, pamoja na kuwajengea uwezo wa kuimarisha uhai wa chama.

“Mafunzo haya yametuongezea vijana wa CCM hali ya kujiamini na kujua majukumu yetu katika kuimarisha chama,” amesema Mpuya.

Naye Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Iringa, Agrey Tonga, amemshukuru Asas kwa msaada wake mkubwa kwa chama, na akamhakikishia kuwa vijana wa CCM wako tayari kutekeleza mafunzo waliyopata kwa vitendo.

“Tutaendelea kumtetea Rais wetu na serikali, na hatutawapa nafasi wapinzani kuichafua CCM,” amesema Tonga.

Pamoja na ahadi zao, Jasmin Ng’umbi, mmoja wa vijana walioshiriki mafunzo hayo, alitoa simu nne na vifaa vya kushonea sare za chama, ili vijana waweze kuimarisha shughuli za umoja huo.

“Tutahakikisha kuwa kila mara tunamtetea Rais wetu na kueneza mazuri yanayofanywa na serikali. Hatutaacha nafasi yoyote kwa wapinzani kutafuta mapungufu na kuwachafua viongozi wetu,” ameongeza Ng’umbi.

Habari Zifananazo

Back to top button