Asasi: Uongozi usiwe fursa kiuchumi

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Salim Asas amewafananisha baadhi ya viongozi wa chama hicho na simu yenye bando na isiyo na bando wakati akiwakumbusha kutumia nguvu zilizowaweka katika nafasi walizonazo kukijenga chama hicho.

Aliyasema hayo leo wakati akifunga semina ya siku moja kwa viongozi wa mkoa wa Iringa na wilaya zake iliyotumika kuwakumbusha wajibu wao kwa chama chao wakati wakijipanga kwa ajili ya uchaguzi wa mwakani wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa 2025.

“Tuna viongozi wanafanya kazi kama inavyofanya kazi simu; ikiwa na hela inafanya kazi na ikiwa haina kitu haifanyi kazi. Viongozi hawa wamesahau kwamba uongozi ndani ya CCM ni wakujitolea,” alisema.

Alisema viongozi hao wanaofanya kazi kama simu bado wana fikra zisizo sahihi kwamba ukiwa kiongozi wa nafasi yoyote ndani ya chama hicho basi hiyo ndio ajira yenyewe au fursa ya kupita huku na kule kuomba chochote.

“Kuna viongozi walitafuta nafasi walizonazo wakijua hiyo ni ajira kwao na ni fursa ya kujipatia chochote kutoka kwa wadau wengine bila kufanya kazi. Badala ya kujenga chama viongozi hao wako bize kurudisha fedha walizotumia wakati wa kampeni zao,” alisema.

Aliwaambia viongozi zaidi ya 90 walioshiriki swmina hiyo kwamba kama kuna kiongozi mwenye fikra hiyo na anashindwa kutimiza wajibu wake kwasababu hapati ujira alioutarajia basi afuate taratibu za kuachia nafasi aliyonayo ili ijazwe na wana CCM wengine wanaotambua uongozi ndani ya chama hicho ni wa kujitolea.

“Kama uliona kuwa kiongozi ndani ya CCM ni fursa unajidanganya na unakidhalilisha chama, kama hutambui kwamba unapaswa kuwa na uchumi wako binafsi wakati ukitekeleza majukumu yako ya kisiasa kwa kujitolea pia unakidhalilisha chama na dhana ya uchumi ni siasa,” alisema.

Alisema viongozi wa CCM wa kuchaguliwa katika ngaz zote wanapaswa kutambua kwamba nafasi walizoomba sio za ajira, waziheshimu na wazitumie kuwajibika.

Alisema wakati viongozi hao wakiomba kuchaguliwa kushika nafasi walizonazo walizunguka kila kata na kukutana na wapiga kura kuwaomba kura.

Lakini cha kushangaza alisema nguvu waliyotumia kutafuta kura zilizowapa ushindi walionao haelewi zimekwenda wapi na kwanini hazitumiki kukijenga chama hicho kwa kukitafutia wafuasi na wanachama wengi zaidi.

Aliwataka viongozi hao kuwajibika ipasavyo kwa kukipigania chama chao kwa hali na mali ili kiendelee kujipatia ushindi mkubwa katika chaguzi zinazokuja.

Semina hiyo ya siku moja ilifunguliwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa Daudi Yasin aliyewalisha kiapo cha kukubali kuyatumia katika kazi zao za kila siku yale
yote watakayojifunza.

Baadhi ya viongozi hao akiwemo Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mko wa Iringa Tumaini Msowoya na Katibu Mwenezi wa CCM wilaya ya Mufind, Dickson Villa wametoa mwito kwa viongozi wenzao kuongeza nguvu ya kukijenga chama hicho kwa kuanzia ngazi ya mashina.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button