Asilimia 50 watoto hatarini afya ya akili

ASILIMIA 50 ya watoto nchini wapo hatarini kukumbwa na matatizo ya afya ya akili wakifikia umri wa utu uzima.

Kwa mujibu wa Msaikolijia Tiba na Ushauri Nasihi Shuleni, Saldin Kimangale, hofu hiyo inatokana na kubainika kuwa, asilimia 50 ya watu wazima waliogundulika kuwa na matatizo ya afya ya akili sasa, waliyapata utotoni wakiwa na umri wa chini ya miaka 14, lakini hawakutambuliwa.

Amesema ili kudhibiti hali hiyo, serikali inapaswa kuweka mkakati wa kuajiri mwalimu wa saikolojia katika kila shule nchini, kwa kuwa shuleni ni rahisi kubaini tabia za watoto ikiwa ni pamoja na mtoto mwenye hali ya huzuni, hasira, utukutu na mienendo mingine ya hatari.

Dk Kimangale, amebainisha hayo wakati wa majadiliano kuhusu  tafiti  mbali mbali  za magonjwa ya Afya ya Akili  katika Kongamano la Nne la  Magonjwa Yasiyoambukiza, jijini Mwanza.

Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Afya Dunia (WHO) ya Mwaka 2021, kujiua ni chanzo cha nne cha vifo vya vijana kuanzia miaka 15 hadi 19.

Profesa Rose Laizer kutoka Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afya na Sayansi Shirikishi (CUHAS) ameshauri kuingiza masuala ya afya ya akili kwenye kadi ya kliniki ya kina mama na kuwe na ushirikiano zaidi baina ya wazazi, walimu, wafadhili, Wizara ya Afya na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ili kumaliza tatizo la afya ya akili.

Naye Profesa Francis Furia kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), amesema matatizo ya afya ya akili huanzia nyumbani, na kutaka wazazi kuacha kuwapa watoto adhabu zilizopitiliza.

Akijikitika katika undani wa changamoto ya afya ya akili kwa watoto, Dk Kimangale amesema kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, Tanzania ina jumla ya watu milioni 61, kati yao takribani asilimia 50 ni watoto chini ya miaka 18, ambao asilimia 50 kati yao wanatarajiwa wawe shuleni.

Amesema tafiti nyingi zinazohusu ukatili wakati wa utoto, zinaonesha kuwa watoto ambao hawapati malezi sahihi ya wazazi na walezi, wapo hatarini zaidi kufanyiwa ukatili, kushuhudia ukatili, kuishi na mwanafamilia mwenye uraibu wa pombe au dawa za kulevya na ufukara

Amesema hayo ni baadhi ya vihatarishi vinavyomuweka mtoto katika hatari ya kupata changamoto ya afya ya akili na hata magonjwa ya akili.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa, mzazi aliyefanyiwa ukatili ana uwezekano mara mbili au zaidi wa kuwa  hatarini kulea watoto kikatili ukilinganisha na yule ambaye hajapitia malezi ya kikatili.

Amesema miaka ya karibu, kumekuwa na taarifa nyingi za watoto kujiua kutokana na sababu mbalimbali na kwamba, hali hii inachochewa na kukosa unasihi.

Amesema baadhi ya watoto wamekuwa wakatili, kupiga wenzao, ukutukutu, kutofuata utaratibu na tabia nyingine mbaya zinatokana na mtoto kupambana na hali ya afya ya akili.

“Hata kwa watu wazima, kuna watu unawaona kazini, lakini wana tatizo la magonjwa ya kiutu na kihaiba; mtu unamuona yupo ‘smart’ lakini anachukua vitu vya wengine; hawezi kuona kitu akaacha, wengine wanawafanyia ukatili wapenzi wao, hawawezi kukaa na wapenzi, anacheka dakika mbili, dakika mbili kakasirika,” amesema Dk

Akaongeza: “… Kitu kidogo anagombana na wenzie, kama ana mtoto, kosa dogo atamfanyia ukali kupitiliza, na mara nyingi watu hawa wanatumia fedha nyingi kujipa furaha.”

Amesema miongoni mwa mambo yanayosababisha changamoto ya afya ya akili kwa watoto ni pamoja na kukosa mapenzi ya wazazi na walezi, pamoja na kukosa mahitaji muhimu ya maisha.

“Unakuta mtoto anaenda shule hana mahitaji muhimu, hali ile inampa sonona, au kafiwa na baba yake watu pole watampa mama, au kafiwa na mama pole atapewa baba, watoto ni kundi linaloachwa, nao wanapata msongo wa mawazo wanahitaji watu wa kuzungumza nao na kuwanasihi,” alisema.

Aidha, Dk Kimangale amehoji “Je, walimu wetu wanayo maarifa na ujuzi sahihi kuhusu magonjwa ya akili na namna ya kutoa japo huduma ya kwanza? …. Je, katika shule zetu tunao utaratibu wa kutambua na kutunza kumbukumbu kuhusu watoto wanaopitia changamoto za afya ya akili?”

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x