Ushirikishwaji mikopo halmashauri wahojiwa bungeni

DODOMA; Serikali imesema inatambua umuhimu wa kuwashirikisha wabunge wote, wakiwemo wa Viti Maalum, katika utoaji na usimamizi wa mikopo ya asilimia 10 katika halmashauri.
Kauli hiyo imetolewa na Niabu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Festo Dugange, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Devotha Mburarugaba, aliyehoji serikali ina mpango gani kuhakikisha wabunge wa Viti Maalumu wanashirikishwa katika utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwenye halmashauri.
“Kufuatia maboresho ya sheria, kanuni na mwongozo wa utoaji na usimamizi wa mikopo hiyo wa mwaka 2024, serikali imeweka utaratibu wa ushirikishwaji wa waheshimiwa wabunge kuhusu hatua za utoaji mikopo.
“Chini ya utaratibu huo, waheshimiwa wabunge wanatakiwa washirikishwe kikamilifu kupitia vikao vya kisheria vya halmashauri, hususan Baraza la Madiwani na Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango ambapo hupokea taarifa, kujadili na kutoa maoni kuhusu upangaji, ugawaji na usimamizi wa mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
“Aidha, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI imewaelekeza wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa kuwataarifu na kuwaalika waheshimiwa wabunge kushiriki kwenye hafla za utoaji mikopo katika halmshauri zao ili kuwapa fursa ya kuhamasisha, kuelimisha na kufuatilia shughuli za vikundi kutokana na mikopo hiyo.
“Mheshimiwa Spika, serikali inazisistiza halmashauri zote nchini kuendelea kuimarisha utaratibu wa mawasiliano na kuwapa taarifa kwa wakati waheshimiwa wabunge kuhusu ratiba za vikao,orodha ya wanufaika na mwenendo wa urejeshaji wa mikopo ili kuongeza uwazi na uwajibikaji,” amesema Naibu Waziri.



