Asilimia 80 nishati safi fursa kiuchumi

DAR ES SAAM: Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dorothy Gwajima, amesema upatikanaji wa nishati safi ya kupikia ni ajenda ya kimkakati inayochochea ukuaji wa uchumi wa taifa.
Amesisitiza kuwa Shirika la Umeme Tanzania, lina wajibu wa kuhakikisha umeme unapatikana kwa uhakika ili kupunguza gharama za kaya, kuongeza uzalishaji na kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Amesema kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2022, asilimia 81 ya kaya bado zinatumia kuni na mkaa kupikia, hali inayosababisha madhara ya kiafya na uharibifu wa mazingira wenye athari za kiuchumi ,ameeleza kuwa serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imelenga kufikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ifikapo mwaka 2034, hatua itakayoongeza matumizi ya umeme na kukuza mapato ya sekta ya nishati.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania, Lazaro Twange, amesema wanaendelea na mipango ya kuwezesha wananchi kupata majiko ya umeme kwa utaratibu wa kulipa kidogo kidogo kupitia ununuzi wa umeme,amesema hatua hiyo itapanua wigo wa watumiaji wa umeme na kuongeza mzunguko wa fedha katika uchumi.

Naye, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa Shirika la Umeme Tanzania, Margath Mwandu, amesema ushirikiano na taasisi za fedha utarahisisha upatikanaji wa majiko ya umeme kwa wananchi wa kipato cha chini,amesisitiza kuwa matumizi ya nishati safi ni mkakati wa kuinua uchumi, kulinda mazingira na kuboresha ustawi wa jamii kwa muda mrefu.



