ASILIMIA 84 ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka 2023 kwa shule za serikali wilayani Biharamulo hawajaripoti shuleni, huku Mkoa mzima wa Kagera walioripoti shuleni kidato cha kwanza ni asilimia 46.
Kutokana na hali hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Angellah Kairuki amewataka viongozi mkoani Kagera kuangalia sababu ya hali hiyo, wakati serikali imepunguza mambo mengi yaliyokuwa yanasababisha wanafunzi washindwe kuripoti.
Kupitia kikao kazi cha tathimini ya utekelezaji wa mkakati wa elimu na uwekaji wa mpango kazi wa utekelezaji kwa mwaka 2023, kilichoongozwa na waziri huyo leo, kilionesha kuwa asilimia 63 ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2023 bado hawajaripoti tangu shule zilipofunguliwa Januari 9, mwaka huu.
Alisema Wilaya ya Biharamulo ndiyo inayoongoza kuwa na wanafunzi wengi ambao hawajaripoti, kwani ni asilimia 16 ya watoto waliofika kuanza kidato cha kwanza huku asilimia 84 wakiwa hawajaripoti, ikifatiwa na Wilaya ya Missenyi, ambayo ina asilimia 20 ya walioripoti na Bukoba ina asilimia 43.
Amezitaja Wilaya za Muleba, Manispaa ya Bukoba, Ngara, Kyerwa na Karagwe kuwa zimevuka asilimia 50, lakini bado haitoshi viongozi wanapaswa kutafuta sababu ya waliopo nyumbani wanafanya nini na kwa ni hawajafika shuleni.
“Ndugu viongozi serikali iliweka miundombinu yote ya wanafunzi madarasa na madawati yake shule zetu nyingi kwa sasa zina umeme na maji, sasa kuna maana gani ya kuwepo vyote hivyo na wanafunzi wasionekane?
“Kama kuna vikwazo vikubwa mmeviweka kwa watoto tunaomba viondolewe, watoto wapokelewe kwanza mengine yatafuata, “alisema Kairuki.
Alisema dhana ya kuwa mtoto ataripoti ndani ya miezi mitatu inawaumiza walimu vichwa, lakini pia inamfanya mtoto kutokuwa na kasi ya kuendana na wenzake, hivyo anabaki nyuma kimasomo, hivyo imani hiyo isiwekewe mkazo, badala yake viongozi wawashauri wazazi watoto wao wafike shuleni waanze masomo.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Alberth Chalamila alisema wanafunzi 56,000 walichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2023 na walioripoti ni watoto 27,000 sawa na asilimia 46.
Pia alisema mkoa ulipanga kuandikisha watoto 86,000 wa shule ya awali na waliofika shuleni kuanza masomo ni watoto 71,0000, huku darasa la kwanza watoto waliopangwa kuandishwa ni 86,000 waliofika ni watoto 76,000.