Asiyeunganisha mfumo ni adui yetu-Dk. Mollel

KIBAHA, Pwani: NAIBU Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, amewataka Wasimamizi wa Huduma ya Afya Ngazi ya Jamii wizarani kuhakikisha asilimia 20 ya mifumo ya kiteknolojia ya Afya Jamii iliyobakia inaunganishwa na kuwa jumuishi ifikapo Januari mwakani ili kufikia agizo la Rais Samia Suluhu Hassan kutaka mifumo isomane ili kurahisisha huduma kwa wananchi na kupunguza vifo vya wajazito, mama na mtoto.
Dk. Mollel amesema hayo leo Desemba 10 kwenye Uzinduzi wa Matumizi ya Mfumo wa Afya-Tek Ndani ya Mfumo Jumuishi wa Kidigitali wa Afya Ngazi ya Jamii (UCS) unaomrahisishia mwananchi kupata huduma rahisi na fanisi ya afya kwa kuunganisha taarifa ya maendeleo ya mgonjwa kwenye maeneo makuu matatu (Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (WADA/CHW), Maduka ya Dawa Muhimu (ADDO) na Vituo vya Afya).

“Asiyeunganisha mfumo ni adui yetu wote. Mfuko wetu wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) unapoteza fedha nyingi kwakuwa na huduma nyingi zinazojirudiarudia pasi na ulazima, hii yote sababu ni kutosomana kwa mifumo.
“Mfano, mgonjwa amechukuliwa kipimo kutoka Kitua A lakini kwakuwa huduma hazisomani itamlazimu kurudia kipimo hicho hicho katika Kituo B hivyo kuongeza gharama kwa mfuko,” amesema Mollel.

Mfumo wa UCS unatumia teknolojia ya kisasa iliyounganishwa kwenye kishikwambi kitakachotumiwa na Mhudumu wa Afya Ngazi ya Jamii Tanzania nzima.
Akizungumzia mfumo huo, Mganga Mkuu wa Wilaya (DMO) Kibaha Wilaya, Dk. Wilford Kondo amesema mfumo huu unasaidia kupeleka taarifa sahihi na kwa wakati kwa Ofisi ya Rais TAMISEMI juu ya namna huduma zinavyotolewa ili kuzichakata na kuchukua hatua stahiki.
“Kupitia mfumo huu wa UCS, TAMISEMI watapata taarifa za moja kwa moja, mfano ikitokea rufaa nyingi za damu, wataalamu wetu watafika ili kutambua kuna changamoto gani?,” ameeleza Dk. Kondo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa WAJA Halmashauri ya Kibaha Mji, Batuli Maeno amesema mfumo huu wa kidigitali unarahisisha katika kutoa huduma tofauti na ule wa zamani wa karatasi.
“Mfumo huu unamrahisishia mgonjwa kuokoa muda, kwani rufaa kutoka WAJA inamuwezesha mgonjwa kufika kwenye vituo vya afya na kuhudumiwa kwa wepesi pasi na kukaa kwenye foleni,” amesema.
Naye, Mfamasia wa Duka la Dawa Mlandizi, Steven Bwire amenukuliwa “Mfumo huu unatusaidia wafamasia kuingia katika mfumo ili kupata taarifa za mgonjwa ili kufahamu aiana sahihi ya dawa inayomfaa mteja.

“Mfano, ikiwa mgonjwa ni mtoto taarifa zitatuonesha mtoto huyu yupo kundi gani la chini ya miaka mitano au zaidi na hali yake ya kiafya ipoje? Inapotokea hali yake ni tete tunampa rufaa kwenda kituo vya afya.”
Akielezea chimbuko la mfumo huo, Mshauri wa Afya wa Apotheker, Dk. Suleiman Kimata, amesema mwaka 2019 walianza na Mradi wa Afya na Teknolojia ‘Afya-Tek’ uliojikita na afya ya mama mjamzito, mama aliyejifungua, mtoto chini ya miaka mitano na mtoto balehe,”
“Katika Mradi huu wataalamu walikuwa wanamtembelea mama mjamzito ili kumpa elimu pia kumshauri juu ya afya yake. Kila mara wataalamu wanatoa maelezo juu ya huduma ya kliniki,” amesema
“Pia tulifanya kazi kwa ukaribu na Maduka ya Dawa Muhimu pia Zahanati na Vituo vya afya,”
Mradi huu unahusisha Utatu ambao faida yake kuu ni kupunguza vifo vya kina mama watoto na wajawazito pia kuboresha afya ya vijana balehe.