Samia ataka mifumo ya haki isomane

RAIS Samia Suluhu Hassan, ametaka mifumo ya kutoa haki nchini isomane ili kuepusha vitendo vya rushwa pamoja na wananchi kupokwa haki zao.

Rais Samia ameyasema hayo leo Januari 31, 2023 mjini Dodoma wakati akizindua Tume ya kuangalia jinsi ya kuboresha taasisi za haki jinai.

Tume hiyo inaundwa na Mwenyekiti Jaji Mkuu Mstaafu Othman Chande, Makamu Mwenyekiti Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu, Balozi Ombeni Sefue.

Wajumbe ni Katibu Mkuu Utumishi, Dk Laurent Ndumbaro, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Profesa Edward Hosea, ambaye amewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Omary Issa ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Umeme (Tanesco) na Saada Makungu, ambaye ni Polisi mstaafu.

Mbali na wajumbe hao, wamo pia Baraka Leonard ambaye ni Ofisa Mwandamizi Ofisi ya Rais na Yahya Khamis Hamad, ambaye ni Mkurugenzi wa Utafiti Chuo Kikuu Zanzibar na Rais mstaafu wa Chama cha Wanasheria Zanzibar.

Rais Samia amesema, “Tunataka mifumo yetu isomane, kwamba mtu akikamatwa na jeshi la polisi kisha akitoa maelezo, hayo maelezo DPP ayaone kwake moja kwa moja.

“Polisi asipate muda wa kuibadilisha, au mtu anawekewa kirungu anaambiwa asaini hapa, tuangalie hilo na jaji hatokuwa na muda wa kuchenga chenga.”

Pia amesema Taasisi ya Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), baadhi ya vijana wake sio waaminifu kwani wamekuwa wakiwabambikizia watu dawa na kuwapa kesi.

“Vijana wetu wanaenda kutegesha wao na kukimbilia kusema mkuu tumekamata hii, kubambika watu kesi, wanachepusha haki za watu, hakuna kitu kibaya kama kuchepusha haki ya mtu, kama wewe hutaki kunyang’anywa haki yako tulinde haki za watu,”amesema.

Amesema katika utendaji kuna mambo kadhaa ya kutizama na katika utendaji wa taasisi za Jeshi la Polisi, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Jeshi la Magereza, na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) hasa katika masula ya mafunzo, ajira na upandishaji vyeo.

“Watu wanapoajiriwa wanapata mafunzo ya kuwapiga brash au ndio wanajikuza wenyewe, system zetu za ajira zipoje, upandishwaji wa vyeo na malalamiko yakoje? Matumizi ya Tehama na ubunifu tupo kwa kiasi gani kwa karne hii ya 21. mifumo isomane, isitoe chance ya watu kuweka mikono,” amesisitiza Rais Samia.

Rais Samia, pia ameitaka Tume hiyo ya Haki Jinai kama itabaini kuna sheria ambazo watadhani  zinatakiwa kubadilishwa basi waseme na waweke na mapendekezo ya nini kifanyike.

 

Habari Zifananazo

Back to top button