Askofu aisifu Taasisi ya Sayansi na Tiba Ndolage

KAGERA; ASKOFU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Magharibi, Dk Abednego Keshomshahara ameisifu Taasisi ya Sayandi na Tiba Ndolage kwa ubunifu na uendelezaji huduma ya afya mkoani Kagera.

Alitoa pongezi hizo wiki hii kwenye mahafali ya 67 ya taasisi hiyo inayomilikiwa na KKKT ambayo wahitimu 62 fani ya uuguzi, uganga, famasia, na ustawi wa jamii walitunukiwa vyeti.

Katika mahafali hayo yaliyohudhuriwa na Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage, Askofu alipongeza uongozi wa taasisi chini ya Dk Eliud Bulaya kwa ubunifu na uendelezaji wake na kufanya izidi kuwa tegemeo kwa maarifa kutokana na chuo na huduma za afya zinazotolewa na hospitali ya Ndolage.

Advertisement

Soma pia: Rais Samia akabidhi ahadi yake ujenzi KKKT Chamwino

Dk Keshomshahara alisema chuo kimeongeza miundombinu ya madarasa na mabweni kukidhi ongezeko la wanachuo.

“Ukarabati wa majengo umefanyika na mazingira yanatunzwa vizuri,” alisema.

 

View this post on Instagram

 

A post shared by HABARILEO (@habarileo_tz)

Alihimiza na kukaribisha vijana wenye sifa kujiunga na kozi mbalimbali chuoni hapo.

Mahafali hayo yaliyohudhuriwa na wachungaji, masista, wainjilisti na wakuu wa vituo vya dayosisi, yalipambwa na burudani ya ngoma ya asili ya Wahaya ambayo Askofu Keshomshahara aliongoza wageni waalikwa akiwamo mbunge Mwijage kuicheza.

Taasisi hiyo kongwe sanjari na kutoa mafunzo ya tiba, inaendesha hospitali maarufu ya Ndolage ambayo imekuwa mkombozi kwa wakazi wa Kagera.