Askofu ataka viongozi wachamungu

ASKOFU Mkuu wa Kanisa Anglicana, Dk Maimbo Mndolwa ametoa wito kwa waumini wa dini zote nchini wenye sifa ya kugombea wakachukue fomu ili kuwapata viongozi wacha Mungu.

Akitoa mahubiri kwenye Ibada ya Msalaba Mtakatifu iliyofanyika Kanisa Anglicana Nambunga lililopo Halmashauri ya Mji Newala mkoani Mtwara, Askofu huyo amesema watu wenye hofu ya Mungu wawe tayari kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ili kuwapata viongozi waadilifu.

“Watu wenye hofu ya Mungu wakishika madaraka wanaongoza kwa unyenyekevu mkubwa na kuweka maslahi ya taifa mbele, wanaposimama katika uongozi kunakuwa na matokeo chanya katika uongozi wao hawajali vyeo vyao wao hujali watu wanaowaongoza kwa haki”

Hata hivyo ametumia ibada hiyo kuwataka viongozi wa dini hizo kutumia vizuri vipindi vya dini mashuleni kuwafundisha watoto ili kuwajenga kiroho na kupata viongozi waadilifu hapo baadaye.

SOMA: Askofu Bagonza aipongeza serikali ujenzi miradi

Mwenyeji wa shughuli hiyo ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi Maalum ambaye pia ni  Mbunge wa Jimbo la Newala mjini, George Mkuchika amewataka waumini hao kuendelea kutii serikali iliyopo madarakani, mamlaka zilizopo duniani kwa sababu mamlaka zote  zimewekwa na Mungu.

Kwa upande wao baadhi ya wakuu wa wilaya mkoani humo akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdallah Mwaipaya amesema viongozi wa serikali wanapaswa kuwa wanyenyekevu katika kuwaongoza watu.

Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, Christopher Magalla amewapongeza waumini wa kanisa hilo kuendeleza umoja na mshikamano kwasababu ndio msingi wa amani na maendeleo kwa ujumla.

Aidha pamoja na mambo menginea Askofu mkuu huyo amefungua jengo la kitega uchumi la kanisa hilo.

Habari Zifananazo

Back to top button