ASKOFU wa Kanisa la KKKT Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza ameipongeza serikali kwa kuhakikisha inarudisha kodi za wananchi kwa kutekeleza miradi ya kisasa ya barabara.
Dk Bagoza ametoa pongezi hizo leo katika uzinduzi wa barabara ya lami yenye mita 700 Kishao Lukajange ambapo amesema serikali imeendelea kuwa na uaminifu wa kukusanya fedha za wananchi na kuzirudisha katika jamii kwa kutekeleza miradi imara ikiwemo barabara nzuri.
Amesema barabara hiyo ambayo inaelekea katika makao makuu ya Dayosisi ya Karagwe imekuwa kiunganishi kikubwa kati ya wananchi na waumini na kuondoa vikwazo kwa wanachi ambao zamani walishindwa kuhudhuria ibada kwa kisingizio cha matope.
SOMA: “Mama ni jasiri na sina mashaka naye”- Bagonza
“Kazi kubwa ya Mwenge wa Uhuru ni kumulika miradi na kuzindua naungana na kila mtu kutambua kazi kubwa ya Tarura, wanafanya kazi nzuri, miradi ya viwango, ombi langu kwa serikali ni kuwa Mwenge wa Uhuru kwa sasa umulike maaadui wetu tulionao ndani ya nchi,”amesema Bagonza.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Godfrey Mnzava akipongeza hatua za manunuzi zilizofanywa na Tarura kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo huku amesema mfumo wa manunuzi wa kidigitali umepunguza mianya ya rushwa na kuweka wazi wadhabuni wenye sifa za kutekeleza miradi ya barabara.
SOMA: Dk Biteko: Rais Samia ni kiigizo cha maridhiano
Meneja wa Tarura Wilaya ya Karagwe, Kalimbula malimi amesema mradi huo umetekelezwa kwa thamani ya Sh milioni 385 lengo likiwa kuboresha huduma za kiuchumi kwa wananchi na kupendezesha eneo la mjini huku chanzo cha fedha hizo ikiwa ni tozo.