Askofu awasihi vijana kudai haki kwa kuzingatia amani

ASKOFU wa Jimbo la Dodoma wa Kanisa la Tanzania Missionary Revival Church (TMRC) Dickson Chiulei amewashauri vijana watakaopata msamaha wa rais kufuatia vurugu za wakati wa Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, mwaka huu, kudai haki zao kwa kufuata utaratibu na si kwa kufanya machafuko na vurugu.

Amesema kitendo cha rais kutoa msamaha huo ni kuonesha dhamira njema na vijana watakaopata huo msamaha wanatakiwa kuuheshimu na kujiepusha na mihemko. Askofu Chiulei amesema hayo jijini Dodoma wakati wa ibada iliyofanyika kwenye kanisa hilo eneo la Area C.

Katika mahubiri yake amewataka vijana kutumia njia zilizo sahihi kikatiba ili waweze kupatiwa majibu na si kwa kufanya vurugu na kuharibu mali za watu na miundombinu mbalimbali. Amesema haki na amani haiwezi kupatikana kwa njia hiyo iliyotumika kwa kufanya vurugu, bali wanatakiwa kuilinda na kuiheshimu kwa kufanya maombi. SOMA: Wazee Tanga waasa vijana

Askofu huyo pia amewataka vijana hao watakaopata msamaha huo wahakikishe wanajishughulisha na utafutaji wa fursa za kiuchumi, ikiwa na pamoja kushiriki katika shughuli za kiroho. “Niwasihi vijana fursa ya kupatiwa msamaha pindi mtakapokuwa huru mzitumie kwa kufanya kazi ambazo zitakazowaletea maendeleo na si mihemko ya kufuata mikumbo isiyokuwa na tija kwa upande wenu vijana,” alisema.

Aidha, amewaomba Watanzania kuungana kwa pamoja katika kipindi hiki kwa kufanya maombi kwa ajili ya kuombea upatikanaji wa haki na amani kwa ajili ya taifa. Amesema haki na amani ndiyo msingi wa kuwepo kwa maendeleo yote ikiwemo na uhuru wa kuabudu bila kuvunja sheria, alihimiza kuungana kufanya dua na kuishi kwa kumtanguliza Mungu kila jambo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button