Nitawanyuka sana – Ateba
DAR ES SALAAM: MSHAMBULIAJI wa Simba, Lionel Ateba ni kama ametuma salama kwa makipa wa timu pinzani kwa kutamka wazi kuwa atafunga sana na kusaidia timu yake kufikia malengo kwa msimu wa 2024/25.
Ateba alianza kuonyesha makeke yake mchezo wa kirafiki wa Kimataifa dhidi ya Al Hilal ya Sudan uliochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita dimba la KMC Complex Mwenge jijini Dar es Salaam.
Katika mchezo huo uliomalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1, Ateba ndiye aliyewatanguliza Wekundu hao wa Msimbazi, kwa shuti kali kwa guu la kushoto akiunganisha krosi iliyochongwa na Ladack Chasambi kabla ya wageni kusawazisha.
Mshambuliaji huyo, amesema tofauti na watu wengi nchini wanavyomfikiria, kwake kufunga mabao ni jambo ambalo amelizoea, hivyo alishangaa kuona baadhi ya mashabiki wakiwa na wasiwasi naye.
SOMA: Ateba ruksa kucheza ligi kuu
Amesema kutokana na upendo na ushirikiano kutoka kwa wachezaji wenzake, wakiwa nje na ndani ya uwanja, anaona atapachika mabao mengi na kuvunja rekodi alizoziweka Ligi mbalimbali alizopita lengo likiwa ni kuipeleka mbali timu hiyo.
“Nimeanza soka langu Tanzania kwa amani na furaha, mechi ya kwanza tu kucheza nimefunga, tena nimefunga dhidi ya timu kubwa, timu ngumu, Al Hilal, nitaendelea kufanya mazoezi kwa bidii, nitaendelea kujituma ili kuweza kushinda mchezo wetu wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahly Tripoli.
“Naamini kwenye mchezo huo nitakuwa vizuri zaidi na tutafanya vema. Malengo ya Simba ni kutwaa makombe msimu huu ndio maana nimesema nitashirikiana na wenzangu kuhakikisha tunapata kile tunachokihitaji,” amesema straika huyo aliyesajiliwa kama mbadala wa Fred Michael.
Amesema ataendelea kufunga mabao mengi zaidi akiwa na Simba anajua mpira sio mchezo rahisi, lakini amekuja kutafuta matokeo, akiwa na furaha akifunga na timu hiyo ikifanikiwa kupata ushindi.
“Ninachowaambia mashabiki wa Simba ni kwamba waje kwa wingi uwanjani kila tunapocheza kutushangilia, msimu huu tunataka kushinda tu, pamoja na kutwaa mataji, jambo zuri ni kwamba kuna ushirikiano mkubwa ndani ya timu,” amesema mshambuliaji.
Ateba, alisubiriwa kwa hamu na wanachama na mashabiki tangu katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Tabora United na wa pili dhidi ya Fountain Gate lakini alishindwa kuonekana kwa sababu za vibali.
View this post on Instagram