Athari mvua za El-nino tahadhari zinapaswa kufuatwa

HIVI sasa mvua zinaendelea kunyesha katika mikoa mbalimbali nchini baada ya mamalaka ya hali ya Hewa Tanzania(TMA) kutangaza uwepo wa mvua za El nino katika Mikoa 14 ambapo kuna uwezekano wa kunyesha kwa asilimia 60.
Mikoa iliyotajwa kukumbwa na El nino ni Pwani,Dar es Salaam, Geita, Tanga,Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Shinyanga, Simiyu, Kagera, Morogoro, Mara,Kigoma na Mwanza.

TMA imesema matukio ya magonjwa ya mlipuko,vifo,uharibifu wa nyumba na miundombinu kutokana na mafuriko na maporomoko ya ardhi vitakuwepo kuanzia Oktoba hadi Disemba,2023.

Mvua hizo ni matokea ya mabadiliko ya tabianchi ambapo mabadiliko hayo yamefanya kuwa na hali tofautitofauti ikiwemo mvua kubwa,ukame,kimbunga,kubadilika kwa misimu na joto kali.

Athari za mabadiliko ya Tabianchi ni pamoja na njaa,magonjwa,uchumi kudorora baada ya shuguliza za uzalishaji kukwama,vifo na watu kuhama makazina.

Sasa ulimwengu umeingia rasmi katika kipindi cha El Niño, kulingana na Shirika la Sayansi la Marekani NOAA, Shirika la Hali ya Hewa Ulimwenguni (WMO) na Umoja wa Mataifa.

Kila nchi kupitia Mamlaka zake za Hali ya Hewa zimeanza kutoa taarifa ya tukio hili la asili linalotokea kila baada ya miaka kadhaa baada ya kuonekana kwenye mifumo yao ya hali ya hewa.

Taarifa ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) ilieleza kunyesha kwa mvua hizo nyingi katika nchi za Afrika Mashariki, Kusini mwa Afrika, Mashariki ya mbali na Amerika ya Kati.

Mvua hizo ambazo zimekuwa zikinyesha kila baada ya miaka miwili na kwa mara ya mwisho nchini zilinyesha mwaka 2016 na kusababisha madhara yakiwemo mafuriko.

Kaimu Meneja Ofisi Kuu ya Utabiri TMA, Dk Mafuru Biseke anasema mifumo ya hali ya hewa inaonesha joto la Bahari ya Pasifiki kuongezeka katika eneo la kati na kuonesha uwezekano wa kunyesha kwa mvua hizo.

Anasema uwepo wa El Nino kutokea unategemea na kukubaliana kwa mifumo iliyopo sasa na mingine na iwapo itanyesha kwa mvua hizo.

Kutokana hilo kamati za maafa ya Mikoa na wataalamu wameandaa namna ya kukabiliana hali ya mvua hizo.

ATHARI ZA EL-NINO

Mvua za mara kwa mara zinaendelea kunyesha katika jiji la Dar es Salaam ambapo hali hiyo inaonesha kuwa utabiri uliotangazwa na TMA unaendelea kutimia.

Katika Mahojiano Maalum na Gazeti la HabariLEO Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,Albert Chalamila anaeleza kuwa wameweka mikakati ya kukabiliana na mvua za el nino ambapo anasema mvua hizo ni moja wapo ya sifa ya mabadiliko ya tabianchi kubwa au pungufu.

“Ulimwengu unakuwa hauna usawa kwasababu vitu ambavyo vinaleta usawa ya ulimwengu vinakuwa vimeharibiwa na shughuli za binadamu na mabadiliko ya tabianchi yanapotokea kuna mambo mengi,”anabainisha.

Anaongeza “Tunafikiri ni nini kinaweza kutokea kama mkoa wetu utakuwa na mvua nyingi? kwanza italeta uharibifu wa barabara, pili uharibifu wa miundombinu nyingine ikiwemo umeme ,maji na mingine kama majengo
Chalamila anasema kuwa mvua nyingi pia zinasabababisha mafuriko na kujaa kwa mito ambayo mwisho wa siku maji yataenda kwenye makazi ya watu kwahiyo kama hayo yakitokea wanasema hizo ni athari.

Ila athari zaidi anaeleza kuwa ni pale ambapo hayo yanapelekea vifo,kuharibika kwa majengo,kukatika kwa madaraja na mengine.

WALIVYOJIPANGA

Jambo la kwanza ambalo Chalamila analianisha ni kutoa elimu kwa umma kuhusu uwepo wa mvua nyingi ili kina mmoja kwa namna alivyo aweze kuhakiki nyumba yake bati,matofali na miundombinu nyingine ili mengine wananchi wanajiandaa.

Chalamila anasema pia kuna maandalizi ya kisaikolojia ambapo lazima mtu ajue kwamba kama kutakuwa na mvua atunze chakula kiasi gani.

Pia wamehakikisha kwamba wanatayarisha mapito ya maji yasiwe na mkwamo kama kuzibua mitaro pamoja na kuhakikisha maji yote yanaelekezwa mahali ambapo hayataleta athari kubwa ambapo mito imesafishwa,kuzibua mitaro na mengine.

“Tumebomoa baadhi ya majengo yaliyojengwa katika baadhi ya miundombinu inayopeleka maji mtoni Kwahiyo hizi jitihada zote tumeanza kufanya kuhakikisha kupunguza maji ambayo ni mengi yasiweze kuleta athari,”anasema.

Pamoja na hayo ujenzi wa madaraja na barabara umekuwa ule wa viwango ili kukabiliana na majanga ambapo muundo wa sasa zinastahimili mafuriko.

“Lakini pia na hali itokanayo na majanga mengine tumekuwa na muundo mzuri wa madaraja yanayoweza kuwa na uwezo mkubwa wa kubeba maji yanayoweza kuleta madhara kulingana na mabadiliko ya tabia nchi,”anasisitiza.

TAHADHARI ZA KUCHUKUA

Chalamila anatoa tahadhari wakati huu wa mvua nyingi watu kuepuka kuvuka sehemu za maji mengi bila uangalifu hasa kwa watu ambao wamelewa kwani watasombwa na maji.

“Kuna Waendesha magari anaona maji mengi na anatavuka kumbe maji yamekata daraja ,watoto wamezoea kuona maji na kuogelea kumbe ndo wanasombwa kwahiyo tunawapa elimu endelevu kwa makundi ya watu wanaopenda pombe,watoto wadogo ,kinamama,madereva na mengine wachukue tahadhari,”anasisitiza.

Aidha anasisitiza kuwa wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi yanayoweza kukumbwa na mafuriko waweze kutoka na kuhamia maeneo salama kwao.

“Watu wote wanaoishi katika maeneoa hayo mfano bonde la mto msimbazi,karibu na bonde la mto mpiji,mlalakuwa ,bonde la mto Tegeta,mto Ngombe wote hawa tumeshakaa kuwahamasisha kwamba maeneo hayo ni hatarishi sasa ni muda mwafaka wa kufanya makazi yao mahali pengine ambapo hapana mafuriko,”anaeleza Chalamila.

Anaongeza “Swali ni je wanamtaji kwa nyumba zao kuvunjwa? na kwenda kujenga maneo mengine? Ninachojua elimu hii hatujaanza kutoa leo ni muda mrefu na utakumbuka eneo la Hananasifu kuja magomeni huu upande wote la mto msimbazi tayari zamani kulishakuwa na watu wamejenga na tayari kulishabomolewa mpaka jangwani nyumba zilishaondelewa.

“ Lakini wale wachache waliopo hadi pembezoni mwa mto Ng’ombe wote hao tulisha waambia muda mrefu tunategemea kuwa hakuna mtu atakayepima kina cha maji tayari wamelishambiwa ili kufanya mambo kuwa mazuri.

Chalamila anasema wananchi wanaokaa kuanzia Tegeta ndevu ,kibaoni,Kibo na Bunju mwisho eneo lote hilo linapokea maji kutoka milima ya Chasimba na chatembo ambayo milima inayokinga kiwanda cha Twiga simenti wamepatiwa elimu na fedha zimetolewa kuhakikisha kuna miundombinu mikubwa ya kutengeneza miferi mikubwa maji yanayotoka katika milima hiyo.

Anabainisha kuwa hiyo ni pamoja na kuwaelekeza wananchi wote waliojenga kwenye mapitio ya maji kuanza kuruhusu njia ya maji haraka iwezekanayo.

Aidha tahadhari zingine ni wananchi kufuatilia utabili wa Hali ya Hewa unaotolewa na Mamlaka husika saa 24 siku 5, Siku 10 na Siku 30 na kuzingatia ushauri unaotolewa.

Lingine ni kuepuka kukaa, kutembea sehemu hatarishi kama kwenye mikondo ya maji na umeme hasa kipindi cha mvua na upepo mkali,wakati wote kuwa na akiba ya chakula, fedha, maji, dawa na vifaa vya huduma ya kwanza (First Aid Kit).

Kuwa na mawasiliano ya watoa huduma za dharura, ya majirani zako na ya kiongozi wako wa eneo unaloishi,toa taarifa kwa Mamlaka inapotokea dharura yoyote katika eneo lako unaloishi.

ELIMU YATOLEWA

Chalamila anasema pia wametoa elimu kwa watanzania kutunza mazingira kwani yakitunzwa dunia yenye usawa inapatikana kwa kufanya vitu rafiki kwa mazingira ikiwemo upandaji miti.

“Tunatoa elimu kuhusu ujenzi wa miundombinu madhubuti ili kuhakikisha madhara hayawi makubwa Rais Samia hataki kusikia kuwa Mkoa wa Dar es Salaam kuna watu wamepata athari za makusudi wakati viongozi tupo tunatoa elimu ya mara kwa mara na kila siku.

Makala haya yamewezeshwa na MESHA na Ofisi ya Afrika ya IDRC Mashariki na Kusini

Habari Zifananazo

Back to top button