ATM ya kwanza ya kubadili fedha yazinduliwa uwanja wa KIA

ATM ya kwanza ya kubadili fedha yazinduliwa uwanja wa KIA

BENKI ya NMB Jumatatu imezindua mashine ya kutolea fedha (ATM) ya kwanza katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa Kilimanjaro (KIA) yenye uwezo wa kubadili fedha za kigeni kwenda shilingi za Kitanzania.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi, Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna alisema wateja na hata wasio wateja wa NMB sasa wanaweza kubadilisha fedha hadi kiasi cha Dola za Kimarekani 2,000 kwa wakati mmoja.

Fedha hizo zitabadilishwa kwa viwango vya kubadilishia fedha vya Benki ya NMB kwa kujihudumia wenyewe.

Advertisement

“Kwa kuanzia, mashine hii itakuwa ina uwezo wa kubadili Dola za Marekani, Euro za Umoja wa Ulaya na Paundi ya Uingereza kwenda shilingi ya Tanzania,” alisema Zaipuna.

Uzinduzi wa mashine hiyo (FX ATM) ni hatua nyingine muhimu kwa Benki ya NMB ya utoaji huduma kwa Watanzania wanaosafiri kutoka nje, watalii na wageni wengine wanaokuja nchini Tanzania.

Uwapo wa mashine hiyo umelenga kuboresha huduma za ubadilishaji wa fedha uwanjani hapo ambapo mteja atakuwa na fursa ya kujihudumia mwenyewe kwa saa 24.

Alisema uzinduzi huo ni muendelezo wa huduma hizo zilizozinduliwa kwa mara ya kwanza na taasisi hiyo jijini Dar es Salaam kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere na kwamba benki hiyo inatarajia kupeleka huduma hizo maeneo mengine ikiwemo Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa Abeid Amani Karume (AAKIA), Kiwanja cha Ndege Zanzibar (Zanzibar Airport) na Zanzibar Stone Town.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu alipongeza uamuzi wa benki ya NMB kwa kuanzisha huduma hiyo ambayo alisema imekuwa ikisubiriwa muda mrefu na wakazi wa mkoa huo hususani wafanyabiashara.

“Huduma hii ni faraja kubwa sana kwetu kwani tunapokea wageni wengi sana na wana uhitaji mkubwa sana wa kubadili fedha za kigeni hivyo hii imekuwa jambo jema sana kwa mkoa wetu na hasa katika kipindi hiki ambacho Royal Tour iliyoasisiwa na Rais Samia Suluhu Hassan imezaa matunda mengi sana,” alisema Mkuu huyo wa mkoa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa KADCO ambayo inaendesha shughuli katika uwanja wa KIA, Christina Makatobe, alisema huduma hiyo ni muhimu kwa taasisi hiyo haswa ikitiliwa maanani KIA ni lango la kuingilia wasafiri kwa wingi wengi wao wakiwa ni watalii.

Naye Mwakilishi wa Benki Kuu nchini (BoT) katika hafla hiyo, Ernest Ndunguru alisema uzinduzi wa ATM za kubadilishia fedha za kigeni kitakuwa kivutio cha watalii wengi nchini kutokana na ukweli huduma bora haswa za kifedha ni moja ya vigezo ambavyo watalii hufuatilia kabla ya kutembelea nchi husika.

 

 

/* */