Aweso: Ufinyu wa bajeti kikwazo miradi ya maji

DODOMA: Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema miradi mingi ya maji ilishindwa kufanikiwa kutokana na ufinyu wa bajeti lakini katika kipindi kifupi cha miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu bajeti ya wizara ya Maji imeongezeka na kusaidia miradi mingi ya maji kukamilika na wananchi kupata huduma ya maji safi na salama.

Aweso ameyasema hayo leo Machi 22, 2024 katika wiki ya kilele cha maji duniani yenye kauli mbiu ‘Uhakika wa Maji kwa Amani na Utulivu’ kwa Tanzania maadhimisho yanafanyika katika ukumbi wa mikutano Mtumba mjini Dodoma.

Aweso amesema, kazi ambayo ilitakiwa kufanyika kwa zaidi ya miaka 10 lakini Rais Samia ameweza kuifanya kwa kipindi cha miaka mitatu .

Advertisement

“Amegawa magari ya uchimbaji visima vya maji na mabwawa ili kurahisisha zoezi la upatikanaji ya maji katika maeneo yote nchini hivyo kama watendaji wa wizara hii tunao wajibu wa kumheshimisha sana Rais Samia Suluhu,”amesema.

Aidha, Aweso amesema Wizara ya Maji kipindi cha nyuma ilikuwa ni wizara ya lawama na kero na hata bajeti za wizara hiyo zilikuwa ni ngumu kupita bungeni lakini toka kuingia kwa Rais Samia ambapo Machi 22, 2021 alipotoa maelekezo yake bungeni juu ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata maji wamejitahidi kwa kiasi kikubwa kutekeleza hilo na ndio maana sasa sekta ya maji inaendelea kufanya vyema.

“Nilipata Mwaliko wako Naibu Waziri Mkuu (Dotto Biteko) siku za hivi karibuni nimeshiriki nawe katika ziara yako tumetembelea vyanzo mbalimbali vya maji zaidi tumekwenda kwenye Bwawa la Ufuaji Umeme la Mwl Nyerere tumeshuhudia umewasha mradi wa umeme na Umeme mwingi umeingia nikuhakikishie Wizara ya Maji itaendelea kushirikiana vyema na Wizara ya Nishati maana wizara hizi ni kama mkulima na mfugaji hivyo zinategemeana sana,”amesema Aweso

Aweso amesema, mradi wa maji wa Same na Mwanga hadi mwezi Juni utakuwa umekamilika kwa asilimia 100 na wananchi wa wilaya hizo wataanza kupata maji na kwamba kwa sasa upo asilimia 86.