Azam FC wimbo ushindi Misri leo

MISRI: KOCHA wa Azam FC, Florent Ibenge, amesema anahitaji kuona kikosi chake kikitafsiri maandalizi mazuri kuwa matokeo uwanjani leo kitakapovaana na ZED FC ya Misri katika mchezo wa kwanza wa raundi ya pili Kombe la Shirikisho Afrika (CAF).
Azam itakuwa ugenini kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cairo ikilenga kupata matokeo yatakayoipa nafasi nzuri kabla ya mchezo wa marudiano utakaochezwa jijini Dar es Salaam Oktoba 24.
Ibenge amewataka wachezaji wake kujiamini na kuingia uwanjani bila hofu, akiamini kuwa wana uwezo wa kupambana na wapinzani wao licha ya kucheza ugenini.
Kauli hiyo inaweka wazi dhamira ya Azam ya kutafuta matokeo mazuri badala ya kuingia Cairo kwa lengo la kujilinda pekee.
Hata hivyo, ZED FC si timu ya kubezwa. Kikosi hicho cha Misri kilianza kampeni yake ya mashindano hayo kwa kuifunga ASAS Djibouti Telecom mabao 4-0 katika mchezo wa kwanza, kabla ya kutoka sare ya bao 1-1 katika marudiano na kufuzu kwa jumla ya mabao 5-1.
Nahodha wa Azam, Lusajo Mwaikenda, amesema kikosi kinafahamu ugumu wa mchezo huo na namna timu za Afrika Kaskazini zinavyoweza kutumia faida ya uwanja wa nyumbani.
Amesisitiza umuhimu wa umakini katika dakika zote 90 ili kuzuia wapinzani wasipate nafasi ya kutawala mchezo.
Kiungo Feisal Salum naye ameeleza kuwa ZED FC ina ubora na wachezaji wenye uzoefu wa mashindano ya kimataifa, hivyo Azam inapaswa kuichukulia kwa uzito badala ya kuhukumu uwezo wake kwa ukubwa wa jina la klabu.
Azam inaingia katika mchezo huo ikiwa na morali baada ya kuifunga Coastal Union mabao 2-0 katika Ligi Kuu Tanzania Bara Oktoba 9. Ushindi huo ni nyongeza ya kujiamini.
Msimu uliopita, Azam ilifanikiwa kufika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, uzoefu ambao inaweza kuutumia katika kukabiliana na presha ya mechi za nyumbani na ugenini. Safari ya kurudia mafanikio hayo inaanza kwa kuhakikisha haiondoki Cairo ikiwa katika nafasi ngumu ya kufuzu.



