DODOMA – SERIKALI imetangaza kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye uingizwaji wa vifaa vya kiteknolojia kwa ajili ya kuwasaidia waamuzi (VAR) ambavyo vitafungwa katika viwanja mbalimbali nchini.
Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba ametangaza hilo jana bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.
Lengo la hatua hii ni kuhakikisha nchi inapata vifaa muhimu vya michezo kwa kuzingatia kuwa, Tanzania ni moja ya nchi mwenyeji zitakazohusika katika maandalizi ya michuano ya fainali ya kuwania Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027 na hivyo kunufaika na ongezeko la akiba ya fedha za kigeni, kukuza taswira ya nchi kimataifa na uwepo wa fursa kwa kampuni za ndani kutangaza biashara zao.
“Aidha, msamaha utatolewa baada ya vifaa hivyo kupata idhini ya Waziri mwenye dhamana ya masuala ya michezo ili kuhakikisha kuwa msamaha huo unatumika kama ilivyokusudiwa na si vinginevyo,” alisema Dk Mwigulu katika hotuba yake.
Tanzania itakuwa mwenyeji wa fainali za Afcon 2027 ambazo itaziandaa kwa pamoja na nchi nyingine mbili za Afrika Mashariki, Kenya na Uganda.
SOMA: Mangungu: Mo ni jasiri
Awali, katika hotuba yake, Dk Mwigulu alisema Serikali ya Awamu ya Sita inatambua umuhimu wa michezo, sanaa na burudani katika kukuza ajira hususani kwa vijana.
Kwa kuzingatia hilo, alisema serikali imeendelea kuwaunganisha wasanii wa Tanzania na soko la kimataifa kupitia mikutano na matamasha mbalimbali na kuhakikisha kuwa kazi za ubunifu wao zinalindwa.
“Aidha, kwa upande wa michezo, Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kujenga misingi ya uibuaji na uendelezaji wa vipaji kuanzia mashuleni ambayo imesaidia kuongeza ajira na kipato kwa wachezaji wanaosajiliwa katika timu mbalimbali ndani na nje ya nchi.
“Kufuatia hatua hiyo ya uendelezaji wa vipaji, imewezesha timu ya taifa ya mpira wa miguu ‘Taifa Stars’ kushiriki mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa mara ya tatu katika historia ya taifa letu na Timu ya Taifa ya Wanawake ya mpira wa miguu ‘Twiga Stars’ kufuzu kucheza mashindano ya WAFCON ambayo yatafanyika mwaka 2024 nchini Morocco,” alieleza Dk Mwigulu.
“Nipende kuwahakikishia kuwa, serikali imejipanga vyema juu ya maandalizi ya michuano hiyo ikiwemo ujenzi wa uwanja wa mpira wa Samia jijini Arusha kama alivyowasilisha Mheshimiwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo,” aliongeza.
Alitoa rai kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuanza maandalizi ya timu ya Taifa mapema ili hatimaye taifa libakize kombe hilo nyumbani.
“Maandalizi ya timu yanahitaji uwepo wa viwanja bora. Serikali imejiandaa kujenga viwanja vipya na kukarabati baadhi ya viwanja vilivyopo. Kuhusu ubora wa eneo la kuchezea yaani pitch kwenye viwanja mbalimbali, tayari serikali ilitunga sheria inayotoa msamaha kwenye uingizaji wa nyasi bandia na vifaa vyake.
“Napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa, msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania tutaanza kutumia ‘’VAR’’ ili kuhakikisha matokeo yanayopatikana uwanjani yanakuwa ya haki maana kuna timu zimezidi – msimu mmoja penalti 10, halafu zikifungwa zenyewe magoli yanakataliwa.
Na ili tuwe na ‘’VAR’’ za kutosha katika viwanja vyote, naleta pendekezo la kutoa msamaha kwenye uingizaji wa mashine za ‘’VAR’’ na vifaa vyake,” alieleza Dk Mwigulu ambaye anafahamika kuwa ni mpenzi wa timu ya Yanga.
Aidha, alizipongeza timu za Azam FC na Coastal Union kwa kufuzu kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika mtawalia mwakani.
Mbali ya timu hizo, alimpongeza mwekezaji wa Yanga, Gharib Said Mohammed (GSM) kwa uwekezaji mzuri alioufanya uliobadilisha taswira na uwezo wa kiuchezaji wa Yanga.
Alisema mafanikio hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na hamasa ya Rais Samia ambaye amekuwa akitoa Sh milioni tano kwa bao linalofungwa katika hatua ya makundi na Sh milioni 10 kuanzia robo fainali, hivyo alimp