Bakwata Katavi waandamana kupinga ukatili wa kijinsia

BARAZA Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Katavi leo machi 22,2023 wamefanya maandamano ya amani lengo likiwa ni kulaani vitendo vya ukatili wa kijinsia, ndoa za utotoni na matendo ya ushoga.

Maandamano hayo yaliyopita maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Katavi yalianzia katika msikiti wa Nuru uliopo katika mji wa zamani na kumalizikia katika msikiti mkuu wa Ijumaa uliopo Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi.

Akizungumza mara baada ya kuwasili katika msikiti wa Ijumaa, Katibu wa BAKWATA Mkoa wa Katavi Omary Muna amesema maandamano hayo ni kuunga mkono juhudi za viongozi wa serikali pamoja na kumuunga mkono Mufti na Sheikh mkuu wa Tanzania Abubakari Zuberi ambapo wanapinga vikali matendo hayo yasiyofaa katika jamii.

“Tunakasirishwa na jambo hili kwa sababu tunatambua hii ni laana ya mwenyezi Mungu, na pindi jambo hili likiendelea kuenea litatuangamiza wote, tutapoteza vizazi vyetu na hatutopata watu ambao watamtambua Mwenyezi Mungu, wote tutakuwa tumemuiga shetani kitendo ambacho Mwenyezi Mungu amekiharamisha na anakikataa”

Kwa upande wake mgeni rasmi Sheikh mkuu wa Mkoa wa Katavi Mashaka Kakulukulu amewataka waislam na wasio waislam mkoani humo kuungana na kukemea vitendo hivyo kwa kuwa watu wanaofanya matendo ya ukatili pamoja na wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja wanaishi nao majumbani na mtaani.

Amesema hawatoishia tuu kwenye maandamano bali watajitahidi kupita maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Katavi ikiwemo maeneo ya Shule na vituo vya kulelea watoto ya yatima ili kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuwa matendo hayo hayakubaliki.

Aidha amewaagiza masheikh wote wa Wilaya mkoani humo kuhakikisha wanaandaa kamati maalumu za makundi mbalimbali yakiwemo ya vijana na wanawake kwa kupata kibali kutoka maeneo husika ambao watapita katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kutoa elimu.

Kwa upande wao baadhi ya waandamanaji wamesema wameungana kwenye maandamano hayo kwa kuwa wanachukizwa na matendo hayo hususani mapenzi ya jinsia moja.

“Hakuna dini ambayo inaruhusu ndoa ya jinsia moja, ikiwa wanadamu tutatambua maana halisi ya ndoa kiundani, tutatambua kuwa mtu gani unapaswa kuishi nae kama mke au mume. Jambo la ulawiti, ushoga, usagaji tutasimama na kulikemea vikali kwa sababu ni jambo ambalo Allah amelikemea vikali” amesema Mudhakir Jafar

Mwisho.

Habari Zifananazo

Back to top button