Bakwata, TEC, CCT wajadili amani

MUFTI wa Tanzania, Shehe Mkuu Abubakar Zubeir, amesema taasisi za dini nchini zimeanza mazungumzo yenye lengo la kuirudisha nchi katika taswira yake kudumisha amani na kulinda maisha na mali za Watanzania.
Katika tamko lake alilotoa jana, Mufti Zubeir amesema mazungumzo hayo yanafanyika yakiongozwa na Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania Nuhu Mruma (BAKWATA). “Mazungumzo hayo tayari yamekwisha anza kupitia Taasisi yetu ya Tanzania Interfaith Partnership (TIP) ambayo kwa sasa Mwenyekiti wake ni Katibu Mkuu wa Bakwata baada ya TEC (Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania) kumaliza muda wake wa mzunguko,” alieleza Mufti Zubeir kwenye taarifa hiyo.
Aliongeza: “Makatibu wakuu wa TEC, Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na Bakwata tayari wamekutana mara kadhaa na hatimaye sisi viongozi wakuu pia tulikutana na mazungumzo yetu yanakwenda vizuri na naamini kwa kuwa sote lengo letu ni kuinusuru nchi yetu na kulinda maisha, mali iwe za umma au za watu binafsi, miundo mbinu na kuirejesha nchi yetu katika taswira yake.”
Shehe Mkuu ameomba wananchi wawape muda viongozi wakuu wa dini waendelee kuzungumza. “Muendelee kuwa watulivu, walinda amani na kuepuka uchochezi wa kutugawa popote pale ulipo uchochezi huo, iwe kwenye mitandao ya kijamii au kwingineko,” alieleza. Ameeleza ni muhimu kuepuka upepo mbaya unaosambaa kwa kasi katika nchi wa chuki za kidini jambo ambalo ni hatari.
“Nawasihi wale wote ambao wanasukumwa na kuhamasisha jambo la fujo, vurugu na uvunjifu wa amani waache kufanya hivyo, siyo tu tarehe 9 au 25 bali siku yeyote ile iwayo kwani kufanya hivyo kunatahatarisha maisha ya watu ambayo yana thamani kubwa,” alieleza Mufti Zubeir.Ameomba Watanzania wawaelimishe wenzao kuhusu madhara ya maandamano yanayokwenda nje ya utaratibu uliowekwa kisheria.
“Kwa upande wa wazazi, tunawaomba tuwape nasaha vijana wetu wasije wakajiingiza kwenye mkumbo na kukubali kutumika kama mtaji wa watu wachache ambao hawaitakii mema nchi yetu,” alieleza Shehe Mkuu. Ametoa wito kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi watumie fursa zao kuisaidia Tanzania badala ya kukubali kutumika kuingamiza nchi yao.
“Wakumbuke kuwa kuipenda nchi ni ukamilifu wa imani. Inawezekana kuwa huko walipo wana hali nzuri ya maisha kuliko Tanzania, lakini wasisahau kuwa nyumbani ni nyumbani tu…Iwapo watakubali kutumika kwa kuiharibu nchi yetu, hasara itakuwa kwetu sote,” alieleza Mufti Zubeir. SOMA: Mtaka: Vijana lindeni amani
Amewasihi wafuasi wa dini na madhehebu yote waunge mkono jitihada za serikali kulinda amani na utulivu kwa kutoa taarifa kwa mamlaka husika iwapo wanafahamu kuna mtu au watu au kikundi cha watu wanapanga au Kkushawishi kufanya vuruho au siku nyingine yoyote



