Balozi azindua kituo mafunzo ya kilimo

BALOZI wa Hispania nchini Tanzania, Jorge Moragas, amezindua kituo maalum cha mafunzo kwa wakulima wadogo wilayani Iringa, ambacho kimepangwa kuanza kutoa mafunzo rasmi mwaka 2025.

Kituo hicho kimejengwa na shirika lisilo la kiserikali la Assisting Small Farmers (ASF) kwa ufadhili wa Shirika la Agronomos Sin Fronteras kutoka Hispania, ambalo limekuwa likifanya kazi katika kijiji cha Mgera, kata ya Kihwele, wilayani Iringa kwa zaidi ya miaka 20 sasa.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi, Balozi Moragas amesema uwepo wa kituo hicho ni sehemu ya mkakati wa kuwainua wakulima wa kata ya Kihwele kupitia mafunzo ya kilimo cha kisasa katika mazao ya mbogamboga, matunda, na nafaka.

Advertisement

Balozi huyo alitembelea pia shughuli za utafiti wa kilimo cha kisasa zinazoendeshwa na taasisi ya ASF, ambapo alipata fursa ya kujionea majaribio ya kilimo cha parachichi, pilipili, na maua yanayofanyika katika kijiji cha Mgera.

Rais wa Agronomos Sin Fronteras, Gabriel Guzman alieleza kuwa lengo kuu la kuanzishwa kwa kituo hicho ni kuhakikisha wakulima na jamii zenye kipato cha chini wanapata ustawi kupitia kilimo bora.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Kheri James, aliipongeza taasisi ya ASF na ubalozi wa Hispania kwa kuwa wabia muhimu katika sekta za kilimo na afya wilayani Iringa akisema kuwa kituo hicho kitakuwa na manufaa makubwa kwa jamii.

“Kuzinduliwa kwa kituo hiki cha mafunzo hapa Mgera kutaleta mageuzi makubwa kwa wakulima wa Iringa na ukanda mzima wa Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania. Tuna uhakika kuwa kituo hiki kitakuwa chachu ya kuzalisha ajira na kuinua wananchi wetu,” alisema Mkuu wa Wilaya James.

Mkurugenzi wa ASF, Dastan Ndunguru, alisema kuwa kituo hicho kitakuwa kikitoa mafunzo kwa wakulima takriban 1,200 kila mwaka juu ya teknolojia rahisi za kilimo cha kisasa, pamoja na kuanzisha kilimo cha mazao mapya yaliyofanyiwa utafiti kwa kuzingatia mahitaji ya soko.

Aliongeza kuwa kwa miaka 20 ASF imekuwa ikifadhili miradi mbalimbali wilayani Iringa, ikiwemo kuhimiza na kuwezesha kilimo cha kisasa, kuwaunganisha wakulima, kuwajengea uwezo, na miradi ya lishe na utunzaji wa mazingira.