Balozi wa China, UNGA na Kanuni ya China Moja

BALOZI wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian anasema miaka 50 tangu kukamilika kwa Reli ya Tazara ni kielelezo muhimu cha uhusiano imara baina ya China na Tanzania.
Anasema hayo hayo anapozungumza na vyombo vya habari ofisini kwake Dar es Salaam na kujikita katika Azimio la 2758 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) na Kanuni ya China Moja akisema lazima ifuatwe.
Kuhusu uhusiano baina ya China na Tanzania kupitia reli hiyo, Balozi Mingjian anasema, “Mwaka huu unatimiza Miaka 50 ya kukamilika kwa Reli ya Tazara inayobeba umuhimu mkubwa wa uhusiano baina ya Tanzania na China.”
Anaongeza: “China iko tayari kuendelea kufanya kazi na Tanzania kama ndugu na washirika wa kweli kuendelea kutekeleza makubaliano ya pamoja yaliyofikiwa na wakuu wa nchi mbili, kuimarisha kuaminiana kisiasa, kuimarisha ushirikiano na mabadiliko, kusaidiana katika kila mambo yanayohusu masilahi kuu na masuala muhimu, pamoja na kujenga jamii ya Wachina na Watanzania zinazoshirikiana katika mambo yajayo”.
Kwa mujibu wa balozi huyo wa China nchini Tanzania, mwaka jana Tanzania na China ziliadhimisha miaka 60 ya mshikamano wa kidiplomasia na kwa kipindi hicho, Kanuni ya China Moja inaunda msingi kuaminiana.
Kwa mtazamo wa China, Balozi Mingjian anasema, “Katika miaka ya 1960 na miaka ya 1970 China ilipokuwa ikikabiliwa na magumu mengi, tulifunga mikanda kusaidia ndugu zetu wa Afrika kujenga Reli ya Tazara bila kusita.”
Anaongeza: “Hii ni kwa kuwa tulijua kuwa Reli ya Uhuru (Tazara) ililikuwa hitaji kubwa la Tanzania na Zambia na harakati zote za ukombozi wa Afrika.” Kwa mtazamo wa upande wa Tanzania, Balozi Mingjian anasema: “Upande wa Tanzania umesaidia China kushikilia kiti chake cha kisheria katika Umoja wa Mataifa (UN) wakati wote tangu kuanzishwa kwa Jamhuri ya Muungano.”
Katika mazungumzo hayo na waandishi wa habari, Balozi Chen Mingjian anamkumbuka Dk Salim Ahmed Salimu aliyekuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa aliyewahi kusema, “Idadi ya watu wa China inawakilisha sehemu moja ya nne ya idadi ya watu duniani, lakini haikuwa na uwakilishi katika UN, hali ambayo ilikuwa kichekesho.
“Dk Salimu alishiriki kuandaa Muswada wa Azimio la 2758 la Umoja wa Mataifa (UNGA) na kuuhitimisha baada ya mapitio kadhaa.” Anasema: “Tanzania kama moja ya waanzilishi na wafadhili muhimu ilichangia vikubwa kupitishwa kwa Azimio la 2758 la UNGA mwaka 1971, lililoanzisha Kanuni ya China Moja kama makubaliano ya kimataifa… Kamwe hatutasahau msaada wa thamani na wa kihistoria wa Tanzania.”
Anaongeza: “Azimio la 2758 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) halitatetereka na Kanuni ya China Moja
lazima ifuatwe.” Anasisitiza kuwa, huo ndiyo msimamo unaosalia kuwa msingi wa sera ya nje ya China.
Azimio la 2758 la UNGA ni nini Kwa mujibu wa Balozi Mingjian, Mwaka 1971 katika Kikao cha 26 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, nchi 23 ikiwamo Tanzania zilishiriki na kupitisha azimio hilo lililolenga kurejesha haki halali ya Jamhuri ya Watu wa China (PRC) katika Umoja wa Mataifa.
Anasema: “Maandishi ya Azimio la 2758 ni mafupi, lakini yenye Uamuzi. Yanaitambua Jamhuri ya Watu wa China kama mwakilishi pekee halali wa China katika Umoja wa Mataifa.” Azimio hili lilipitishwa kwa wingi wa kura na kuhitimisha mjadala wa kimataifa ndani ya mfumo wa Umoja wa Mataifa kuhusu nani anaizungumzia China.
Azimio hilo halikutaja au kufafanua upya maeneo, wala halikusema chochote wazi kuhusu ‘Wachina wawili’ au
‘familia iliyogawanyika.’ Ilikuwa rahisi: “Kiti kimoja, China Moja, Serikali moja na hiyo ni PRC.”
Ili kuelewa mzozo huo ni lazima mtu arudi mwaka 1971. Katika Kikao cha 26 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa zilishiriki nchi 23 ikiwamo Tanzania, na zilishiriki azimio lenye lengo moja: ‘kurejesha haki halali ya Jamhuri ya Watu wa China (PRC) katika Umoja wa Mataifa na kuwafukuza wawakilishi wa Chiang Kai-shek.’
Azimio hili lilipitishwa kwa wingi wa kura na kuhitimisha kikamilifu mjadala wa kimataifa ndani ya mfumo wa Umoja wa Mataifa kuhusu nani anaizungumzia China. Bila kutaja jina, balozi huyo anazilaumu baadhi ya nchi kwa kupotosha kwa makusudi maana na athari za Azimio la 2758 la UNGA.
Kwa Serikali ya China, hatua kama hizo zinapinga mamlaka ya China, zinakiuka sheria za kimataifa na kudhoofisha Umoja wa Mataifa wenyewe na pia, hazihusu maadili ya kidemokrasia au ushirikishwaji wa kimataifa. Anasema, “Kuna China moja tu ulimwenguni.”