Bandari Mtwara yaendelea kuhudumia mizigo

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari (TPA) imesema Bandari ya Mtwara iko imara na inaendelea kuhudumia mizigo ikiwemo shehena ya korosho kwenda nje ya nchi.

Meneja wa bandari hiyo, Ferdinard Nyathi amesema mpaka sasa meli tano zimefika na kupakia shehena ya korosho na kusafirishs kwenda masoko ya nje.

‘Napenda kuwahakikishia kuwa bandari ya Mtwara ina ufanisi mkubwa na inaendelea kufanya kazi vizuri,” amesema.

Advertisement

Nyathi amesema hayo leo wakati akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara pamoja na viongozi wa siasa Mkoani huku waliotembelea bandari hiyo kujionea maendeleo.

‘Kwenye upande wa korosho tunaendelea kuhudumia shehena ya korosho na mpaka sasa meli nyingi zimeshafika kuleta makasha na meli tano zimechukua mzigo wenye tani 79 wa korosho na kusafirisha kwenda nje ya nchi,” amesema.

Nyathi amesema meli nyingine za kubeba korosho zinaendelea kuhudumiwa. Amesema bandari hiyo ina miundombinu na vifaa vyote muhimu vya kuhudumia shehena ambavyo vinapelekea bandari hiyo kupata mafanikio makubwa.

Mkuu wa Mkoa, Kanali Patric Sawala amepongeza juhudi za mamlaka ya usimamizi wa bandari na kusema nia ya serikali ni kuhakikisha kuwa uwekezaji ambao umefanyika katika bandari unaleta manufaa.

‘Serikali imewekeza zaidi ya Sh bilioni 157.8 kwenye bandari yetu ya Mtwara  kwa ajili ya maboresho, na tunafarijika kuona uwekezaji unaleta manufaa, kazi zinaendelea na kama mnavyoona korosho zote zinasafirishwa kupitia bandari yetu,”amesema.