Bandari Tanga yapokea meli ya magari

Bandari Tanga yapokea meli ya magari

BANDARI ya Tanga kwa mara ya kwanza imepokea meli ambayo imebeba mzigo wa magari pamoja na shehena nyingine za mizigo kutoka nchini China.

Meli hiyo ijulikanayo kwa jina la Della, ilipakia shehena ya mizigo katika Bandari ya Zhanjiangang iliyoko Shanghai nchini China na kusafirisha mizigo katika Bandari mbalimbali ikiwemo ya Tanga.

Akizungumza wakati wa upokeaji wa shehena hiyo ya mizigo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba amesema ujio wa meli kubwa za mizigo inatokana na maboresho makubwa yaliyofanyika ya ujenzi wa gati mpya yenye urefu wa mita 450.

Advertisement

“Hii bandari ndio moyo wa uchumi wa Mkoa wa Tanga, hivyo huu ni mwanzo tuu wa ujio wa meli kubwa kwani tutaendelea kuvunja rekodi Kila mara na niwaombe  wafanyabiashara kuitumia bandari ya Tanga kwa ajili ya uhakika wa usafirishaji wa mizigo, “amesema Kindamba.

Naye Meneja wa Bandari ya Tanga, Masoud Mrisha amesema kuwa meli hiyo yenye urefu wa meta 176 imetia nanga katika gati na itaweza kuhudumiwa kwa siku moja pekee.

“Uwepo wa vifaa vya kisasa umerahisisha shughuli za upakuaji wa shehena ya mizigo, ikiwemo kupunguza muda wa kuhudumia shehena katika Bandari yetu,”amesema Mrisha.

1 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *