Barabara kilimani B Kirumba kuanza kujengwa

MBUNGE wa Jimbo la Ilemela Jijini Mwanza, Dk Angeline Mabula amekabidhi mifuko ishirini ya saruji kwaajili ya ujenzi wa barabara ya mtaa wa Kilimani ‘B’ kata ya Kirumba ili kuondoka adha ya usafiri kwa wananchi wa mtaa huo.

Akizungumza wakati wa zoezi la makabidhiano ya saruji hiyo, Katibu wa Mbunge Kanda ya Kirumba, Fatma Karoli amesema kuwa Jimbo la Ilemela limekuwa na desturi ya kufanya kazi kwa utaratibu wa utatu kwa maana ya wananchi kuanzisha mradi, Mbunge kuunga mkono kwa kuuendeleza mradi huo na kisha manispaa au serikali kuu kumalizia kwa kukamilisha mradi husika.

Advertisement

”Mbunge wetu anatambua adha tunayopata Kwa ukosefu wa barabara za uhakika, mlivyoanza akaona awaunge mkono na huu ni utaratibu wake wa kawaida kabisa amefanya hivi kwenye miradi mingi ndani ya jimbo letu” Alisema.

Aidha katika hatua nyingine Bi.Karoli amewaasa wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali chini ya Rais Dk Samia Suluhu Hasan katika kuwaletea maendeleo wananchi pamoja na kumuombea mbunge wao ili aendelee kuwatumikia

Naye mratibu kutoka ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Ilemela Ndugu Mpunzi Mbegeje amesema kuwa Mbunge Dkt Angeline Mabula ataendelea kutatua kero zinazowakabili wananchi wake katika nyanja mbalimbali ikiwemo sekta ya afya, elimu na miundombinu hivyo kuwaasa viongozi wa kata na mitaa kutoa ushirikiano.

Wessa Juma ni diwani wa kata ya Kirumba ambae amemshukuru Mbunge huyo Kwa msaada wa mifuko ya Saruji itakayosaidia ujenzi wa barabara ya mtaa wa Kilimani ‘B’ kwani imekuwa ikiwatesa wananchi wa kata yake kwa muda mrefu kitendo kilichochangia kukwamisha maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi hao kwa kushindwa kufika sokoni na mwaloni Kwa urahisi Ili kufanya shughuli za uzalishaji mali

Umrat Ibrahim Kapera ni mwananchi wa mtaa wa Mlimani ‘B’ kwa upande wake  amewataka viongozi wengine kuiga mfano wa Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Dk Angeline Mabula Kwa jinsi  anavyoshirikiana na wananchi wake katika kutekeleza miradi ya maendeleo na kutatua kero za wananchi hasa adha iliyokuwa ikiwakabili wanawake wajawazito pindi wanapotaka kujifungua kabla ya kuanza kwa ujenzi wa barabara hiyo.