Barabara Kongowe-Kibada Kukarabatiwa mabega
DODOMA; SERIKALI imesema ipo kwenye hatua ya ununuzi ya kumpata mkandarasi wa kufanya ukarabati wa mabega ya Barabara ya Kongowe-Kibada jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ametoa kauli hiyo leo Septemba 7, 2023 alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mbagala, Abdallah Chaurembo aliyetaka kujua serikali ina mpango gani wa kujenga mifereji Barabara ya Kigamboni-Kongowe, Mtaa wa Mikwambe Kata ya Toangoma jimbo la Mbagala.
“Katika mwaka wa fedha 2023/24 Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dar es salaam, ipo kwenye hatua ya manunuzi ya kumpata Mkandarasi wa kufanya ukarabati wa mabega ya Barabara ya Kongowe – Kibada, yenye urefu wa kilometa moja.
“ Ukarabati huo pia utahusisha ujenzi wa mitaro kwenye baadhi ya maeneo, ikiwemo eneo la Mikwambe yenye urefu wa kilometa mbili,” amesema Waziri Bashungwa.