Barabara Kyerwa sekondari yafikia 96%

MRADI wa ujenzi barabara ya Kyerwa Sekondari wenye thamani ya Sh milioni 474  kilomita moja wenye kiwango cha lami umefikia asilimia 96 ya ukamilikaji wake ambapo Novemba mwaka huu utamalizika.

Mwenge wa Uhuru kitaifa umefika na kukagua mradi huo unaoendelea kutekelezwa kwa lengo la kupendezesha mji na kufungua lango la makao makuu ya wilaya ambapo mbio za mwenge huo zimeridhishwa na utekelezaji wa mradi huo.

Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi, Meneja wa Tarura Wilaya ya Kyerwa, Yetron Mbasha amesema   barabara hiyo imekuwa muhimu kwani baada ya kuanza kwa mradi tayari wawekezaji wamejenga viwanda  katika eneo hilo kuna huduma ya shule, na wananchi wamevutiwa kujenga makazi.

“Wakati tunaanza kujenga barabara hii hakukuwa na makazi kabisa ,sasa Kuna makazi,kuna kiwanda kikubwa cha kuongeza thamani kwenye madini ya TIN, kiwanda cha kukoboa kahawa na tayari wananchi wamejenga na wengine kuajiliwa hivyo barabara hii ni muhimu katika kuwaunganisha wananchi kupata huduma,” amesema Mbasha

Akizungumza baada ya kutembelea mradi huo, kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Godfrey Eliakimu Mnzava amesema kuwa ameridhishwa na utekelezaji huo.

“Baada ya ukaguzi tumeridhika kazi inaendelea kufanyika vizuri mwenge wa Uhuru umetembelea na kukagua na baada ya kuyasema hayo mwenge wa Uhuru upo tayari kuendelea na ratiba inayofuata”.

Mbunge wa Jimbo la Kyerwa, Innocent Bilakwate amesema kwa kipindi cha miaka mitatu kuna ongezeko la barabara za lami makao makuu ya wilaya hiyo mpya mpaka kilometa 5 na serikali inaendelea kuongeza jitihada za kutengeneza barabara .

Mradi huo ulianza kutekelezwa Septemba 15, 2023 ikiwa ni mwendelezo wa ujenzi wa barabara makao makuu ya wilaya ya Kyerwa kwa lengo la kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji.

Habari Zifananazo

Back to top button