Barabara Tanzania, nchi jirani kujengwa kwa awamu

SERIKALI imesema inaendelea na ujenzi na ukarabati wa barabara zinazounganisha Tanzania na nchi zote za jirani ikiwemo DR Congo kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ametoa kauli hiyo leo Februari 7, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la mbunge wa Viti Maalum, Felista Njau aliyeuliza Je, kuna mkakati gani wa kuboresha miundombinu katika mipaka ya nchi yetu na nchi jirani zenye fursa za kibiashara kama DR Congo ili kukuza diplomasia ya uchumi.

Aidha, Bashungwa amesema Serikali imekamilisha ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya Sumbawanga  Matai hadi Bandari ya Kasanga (km 107) mkoani Rukwa na tayari imesaini mkataba wa kujenga kwa kiwango cha lami wa barabara ya Kigwira  Karema (km 112) kwenda Bandari ya Karema mkoani Katavi.

Pia amesema Serikali inatekeleza mpango wa kuboresha barabara ya kuanzia Igawa  Mbeya – Tunduru kuwa njia nne.  Pia Serikali inaendelea kuboresha viwanja vya ndege vya Songwe, Sumbawanga na Kigoma ambavyo vipo mpakani na DR Congo.

Kwa upande mwingine,mbunge wa Kwimba, Shanif Jamal alitaka kujua Je, lini Serikali itaanza mchakato wa kutangaza barabara ya Mabuki – Jojiro hadi Ngudu ili ijengwe kwa kiwango cha lami.

Akijibu Swali hilo, Bashungwa amesema Serikali imeanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Mabuki – Jojiro – Ngudu (km 28) kwa kiwango cha lami kwa awamu ambapo mkataba wa ujenzi wa kilometa 3 kuanzia eneo la Ngudu mjini kuelekea Jojiro umesainiwa tarehe 19 Januari, 2024.

Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuendelea na ujenzi kwa kiwango cha lami kwa awamu kwa sehemu iliyobaki.

Habari Zifananazo

Back to top button