Madiwani Mtwara wapitisha bajeti Sh bil 33

BARAZA la Madiwani wa Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara limeridhia na kupitisha rasimu ya bajeti ya Sh bilioni 33.1 kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Akizungumza wakati wa kikoa cha Baraza la Madiwani hao kuhusu kupitisha bajeti hiyo, Diwani wa Kata ya Kisungule Issa Muhamed amesema bajeti hiyo itaenda kutatua kero katika sekta mbalimbali ikiwemo miundombinu ya barabara, elimu, afya, utawala bora na mingine.
Amesema kutokana na kuongezeka kwa mapato katika manispaa hiyo kumepelekea kuongezeka kwa bajeti hiyo na ni imani yake kubwa kuwa itasaidia kufikia malengo ambayo manispaa imejiwekea ikiwa awali yalikuwa hayafikiwi.
Diwani wa Kata ya Naliendele katika manipaa hiyo, Masudi Dali amesema bajeti hiyo itaenda kuimarisha pia miundombinu ya wananchi kama vile ofisi za mitaa na kufanya ukarabati kwa baadhi ya shule ambazo miundombinu yake hairidhishi.
“Bajeti yetu ambayo tumeipendekeza tunakwenda kuimarisha miundombinu ya wananchi kama vile ofisi za mitaa, miundombinu ya madarasa ya shule, madawati na tumeipendekeza shule za pembezoni zikafanyiwe ukarabati wa kutosha kuna shule ya msingi Mkangala, mwenge, lwelu na maeneo mengine’’
Hata hivyo Diwani wa Kata ya Likombe Saidi Salumu amesema kata yake kupitia bajeti hiyo itaenda kutekeleza shughuli za kijamii kwa asilimia 75 hasa miradi ambayo mwazo haikufanikiwa kama vile soko.
“Miradi mingi inayokwenda kutekelezwa katika naeneo yetu kupitia bajeti hii itahakikisha inarudisha mapato kwa serikali”amesema Sslum
Naibu Meya wa Manispaa hiyo,Sigmund John ametoa rai kwa madiwani hao kwenda kutangaza yale yote mazuri yanayofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika mkoani humo na nchi kwa ujumla.



