Baraza la Wafanyakazi lapongeza utendaji PURA

BARAZA la wafanyakazi wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), limeeleza kufurahishwa na mamlaka hiyo kwa kuendelea kuboresha mazingira ya utendeji kazi kwa watumishi wake na kuleta ufanisi katika utendaji wao.

Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE), Mkoa wa Dar es Salaam, Sara Rwezaula, amesema utendaji wa mamlaka hiyo umeendelea kuimarika mwaka hadi mwaka kutokana na mazingira bora ya utendaji kazi.

Sara amesema hayo wakati akizungumza katika kikao cha Baraza la Wafanyakazi PURA kilichofanyika jijini Arusha kwa lengo la kupokea na kujadili taarifa za utekelezaji kutoka idara na vitengo vya taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/22 na robo ya mwaka wa fedha 2022/23.

“Kupitia taarifa tulizozipokea na kujadili, tumeona dhahiri kuwa taasisi imekuwa na utendaji unaoridhisha. Pongezi nyingi pia kwa menejimenti ya PURA kwa kuendelea kuboresha mazingira ya kazi, jambo muhimu katika kufanikisha utendaji,” amesema.

Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi PURA ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka  hiyo, Mhandisi Charles Sangweni, amesema pongezi zilizotolewa ni chachu kwa wafanyakazi wa PURA kuendelea kufanya kazi kwa bidii zaidi, ili kufikia malengo kama yalivyo katika Mpango Mkakati wa PURA.

“Nipende kutumia fursa hii kuwahimiza wafanyakazi wote wa PURA, kuendelea kufanya kazi kwa bidii, weledi na kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma. Tusibweteke kwa pongezi hizi bali ziwe kichocheo kwa sisi kufanya vizuri zaidi na zaidi,” alieleza Mhandisi Sangweni.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button