TABORA – WAZIRI wa Kilimo, Hussein Bashe amewatoa wasiwasi wakulima wa zao la mahindi akisema serikali itanunua kwa bei ya kuridhisha isiyopungua Sh 600 kwa kilo.
Akizungumza na wakulima kwenye kilele cha Siku ya Ushirika Duniani mkoani Tabora jana, Waziri Bashe alisema anatambua kwa sasa watu wananunua mahindi kwa Sh 200, Sh 300 kwa kilo.
“NRFA (Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula) inafungua masoko Julai 10, tutaanza kununua mahindi kwa wakulima na nawaambia najua bei imeanguka kwa sasa… tutaendelea kufanya tathmini namna masoko yanavyoendelea,” alisema.
Kuhusu utoshelevu wa chakula nchini, Waziri Bashe alisema kwa sasa nchi ina utoshelevu mkubwa ikiwa imefikia asilimia 124: “Msimu huu tulioanza kuvuna sasa tutafikia lengo la mwaka 2025/2026 kufikia asilimia 130 mwaka mmoja kabla,” alisema.
“Hiyo maana yake ni kwamba utoshelevu wa chakula kwenye nchi yetu tuna zaidi ndio maana hivi karibuni tulisaini mkataba wa kuiuzia Zambia mahindi tani 650,000 ambazo nchi itaingiza faida ya Dola za Marekani zaidi ya milioni 220 (zaidi ya Sh bilioni tano),” alisema.
Kuhusu zao la tumbaku, Bashe alisema serikali imetoa Sh bilioni 13 kwa ajili ya ruzuku kufidia hasara ya gharama zao za uzalishaji kutokana na mvua za El Nino lakini hatotoa fedha hizo mpaka utaratibu uliowekwa ufuatwe.
“Nataka nipate jina la mkulima, namba ya kuuzia kwenye chama cha msingi, jina la Amcos yake, idadi ya mifuko ya mbolea aliyonunua, akaunti yake ya benki ili fedha alipwe mkulima moja kwa moja sitatoa fedha bila kupata vitu hivyo,” alisema.
SOMA: ‘Serikali yawatoa hofu wadau nishati safi ya kupikia’
Aliitaka Bodi ya Tumbaku ikutane na Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCJE) kutengeneza mkeka wa majina hayo ya wakulima na kuuwasilisha kwa waziri mchakato wa malipo uanze.
“Pia Rais ameidhinisha shilingi bilioni 13.3 kusaidia kupunguza gharama za pembejeo kwenye msimu unaokuja wa wakulima wa tumbaku, safari hii mbolea yote ya tumbaku imeagizwa na serikali kupitia TFC (Kampuni ya Mbolea Tanzania)… mbolea ipo na tutaanza kuisambaza kabla ya mwezi wa nane”.
“Pia alisema wameshaanza kufanya tathmini ya mali za vyama vya ushirika na mpaka sasa wamefikia asilimia 50 ya vyama vyote na kuwa na mali za thamani ya Sh trilioni nne,” alisema.
Kuhusu sukari alisema baada ya Rais kusaini sheria mpya na yeye ameshasaini kanuni hivyo hakuna Mtanzania atakayekula sukari kwa zaidi ya Sh 3,000 kwa kilo.