Bashungwa asifu Polisi weledi mikutano ya CCM, Chadema

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa ameeleza kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kutekeleza jukumu lake la kikatiba kwa kusimamia usalama katika mikutano na shughuli za vyama vya siasa bila kujali itikadi ya chama cha siasa chochote.

Amelipongeza jeshi hilo kwa kusi[1]mamia ulinzi na usalama kwa vyama vyote vya siasa kwa weledi katika Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama Cha Mpinduzi (CCM) uliofanyika Dodoma pamoja na Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Chama cha De[1]mokrasia na Maendeleo (CHADEMA) uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Bashungwa alisema hayo jana ali[1]pofanya ziara ya kikazi makao makuu ya Jeshi la Polisi, Dodoma ambako alisisitiza vyama vya siasa kutimiza wajibu wa kutii sheria bila shuruti ili kuepuka kulazimishwa kutii sheria.

Advertisement

“Matarajio yangu ni kwamba haki hii mnayoitenda Jeshi la Polisi kwa kutoangalia itikadi, pia vyama vya siasa vya upinzani na vyama vya siasa kwa ujumla, ije na wajibu kwa wao kutii sheria bila shuruti, hakuna haki bila wajibu,” alieleza.

Aliliagiza jeshi hilo kujipanga kusimamia kikamilifu usalama kwa raia na mali zao wakati wa uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka huu, kuendelea kudumisha usalama, amani na utulivu wa nchi. Awali, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IJP Camillus Wambura alieleza kuwa jeshi hilo limejiimarisha vyema kwa kuweka mikakati thabiti ya kuimarisha usalama kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu.