Bashungwa awapa raha Wananchi Mpwapwa

DODOMA; Waziri Ujenzi, Innocent Bashungwa amewahakikishia Wananchi wa Wilaya Mpwapwa kuwa Serikali ipo mbioni kusaini mkataba wa ujenzi kwa kiwango cha lami Barabara ya Kongwa Jct- Ng’ambi -Mpwapwa yenye kilometa 32.
Bashungwa ameeleza hayo kwa njia ya simu wakati alipotakiwa kutoa ufafanuzi na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM Taifa – UWT, Mery Chatanda wakati akiongea na wananchi katika ziara yake wilayani Mpwapwa.
“Ujenzi wa kiwango cha lami wa barabaa ya kuunganisha Wilaya ya Kongwa na Mpwapwa imegawanywa katika sehemu mbili, sehemu ya kwanza ni km 32 ambayo tumeshampata mkandarasi Estim Construction Company ambapo mkataba utasainiwa hivi karibuni” amesema Bashungwa.
Aidha, Bashungwa ameeleza pia Barabara ya Mpwapwa- Gulwe -Kibakwe yenye Kilometa 46 ipo katika hatua ya manunuzi kwa ajili ya kumpata Mkandarasi wa kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Ameeleza kuwa Rais, Samia Suluhu Hassan anafahamu kilio cha wananchi hao na ameshatoa maelekezo ya kuhakikisha barabara hizo mbili muhimu zinajengwa kwa kiwango cha lami.
Nae, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM Taifa – UWT, Merry Chatanda amemtaka Waziri Bashungwa kuhakikisha mikataba hiyo ya ujenzi wa barabara hizo unasainiwa mbele ya wananchi pindi taratibu zitakapokamila.
12 comments

Comments are closed.