MANYARA: Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema kazi ya kuondoa tope inaendelea na shughuli kubwa inayofanyika kwa sasa ni kufungua mitaa yote ya mji wa Katesh na kurejesha mji katika hali yake ya awali kwa kuwezesha shughuli za uzalishaji kuendelea.
Ameyasema hayo mapema leo wakati wakikagua kazi zilizofanyika ambapo aliambatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama, Waziri wa Madini, Antony Mavunde na Viongozi wengine Desemba 6, 2023.
“Maelekezo ya Rais, Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha leo kufikia usiku, mji wa Katesh na mitaa yake iwe imesafishwa ili kushughuli za uzalishaji ziendelee kama mnavyoona wafanyabiasha wameanza kufungua Maduka” amesema Bashungwa.

Bashungwa amesema TANROADS kwa kushirikiana na TARURA tayari wameweka mpango kazi wa pamoja ambao utahakikisha kazi hiyo inaendelea kufanyika usiku na mchana mpaka shughuli hiyo itakapokamilika.
Aidha, Waziri Bashungwa amevipongeza vyombo vya ulinzi na usalama, kwa kazi kubwa wanayofanya ambapo wamehakikisha wanaleta vijana wa JKT wanaoshiriki katika zoezi la uokozi ikiwa ni pamoja na kusaidia kazi za kurejesha hali nzuri katika mji wa Katesh.

Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama amesema kuwa wanaendelelea kutekeleza maagizo ya Rais Samia ambayo jambo la kwanza lilikuwa ni kukabiliana na mafuriko na kuhakikisha matibabu kwa wahanga yanatolewa bure.