BEI ya mafuta ya petroli na dizeli kwa jumla na rejereja kwa Januari, 2025 imeendelea kushuka kulinganisha na Desemba 2024.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Dk James Mwainyekule, bei mpya ya mafuta ya petroli kwa rejareja lita moja itauzwa kwa Sh 2,793 ukilinganisha na bei ya Desemba ambapo lita moja iliuzwa Sh 2,898.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, bei ya mafuta ya dizeli yanayopita katika Bandari ya Dar es Salaam kwa rejareja nayo imepungua kutoka Sh 2,779 Desemba 2024 hadi kufikia Sh 2,644 Januari 2025.
Kwa mafuta yanayopitia katika Bandari ya Dar es Salaam bei za mafuta kwa jumla pia zimepungua ambapo petroli itauzwa Sh 2,662 ikilinganishwa na Desemba ambapo bei ya petroli ilikuwa Sh 2,767.
Kwa bei ya mafuta ya dizeli yanayoingia kupitia Bandari ya Dar es Salaam bei imepungua kutoka Sh 2,647 Desemba hadi kufikia Sh 2,513 Januari 2025.
Kwa bei za mafuta ya rejareja yanayoingia kupitia Bandari ya Tanga, petroli imepungua kutoka Sh 2,905 kwa lita hadi Sh 2,800 kwa lita huku dizeli imepungua kutoka Sh 2,792 hadi Sh 2,656 na mafuta ya taa yamepungua kutoka Sh 2,877 na sasa yanauzwa kwa Sh 2,722.
Kwa bei za mafuta za rejareja yanayoingia kupitia Bandari ya Mtwara petroli imepungua kutoka 2,908 hadi Sh 2,866 na dizeli imepungua kutoka Sh 2,851 hadi kufikia Sh 2,716 huku mafuta ya taa bei imepungua kutoka Sh 2,903 na sasa yakiuzwa kwa Sh 2,748.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, bei hiyo gharama za uagizaji mafuta zimeongezeka kwa wastani wa asilimia 5.4 kwa petroli, asilimia 13 kwa dizeli na wastani wa asilimia 8.8 kwa mafuta ya taa katika Bandari ya Dar es Salaam.
Hata hivyo gharama za uagizaji kwa aina za mafuta zimepungua kwa asilimia 6.6 kwa petroli na asilimia 6.67 kwa dizeli katika Bandari ya Tanga.
Na zimepungua kwa wastani wa asilimia 4 kwa mafuta ya petroli na asilimia 10 kwa mafuta ya dizeli katika Bandari ya Mtwara