BELARUS: Lukashenko kuongoza muhula wa saba

BELARUS : MTAWALA wa kimabavu wa Belarus, Alexander Lukashenko, ameendelea kutawala nchi hiyo kwa kushinda muhula wa saba mfululizo madarakani, licha ya kushutumiwa na Umoja wa Ulaya na wapinzani wake wanaoishi uhamishoni au magerezani.

Lukashenko, ambaye ameiongoza Belarus tangu mwaka 1994, alitangaza ushindi katika uchaguzi ulioibua maswali mengi kuhusu uhalali wake.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni ya waliopiga kura, mtawala huyo mwenye umri wa miaka 70 alionekana kushinda kwa asilimia 87.6 ya kura, ushindi ambao umekuwa ukikosolewa vikali.

Kama ilivyokuwa kwenye uchaguzi wa 2020, Lukashenko ameendeleza mkakati wa ukandamizaji dhidi ya wapinzani wake, akiwakamata na kuwafungia wengi wao.

Hata hivyo, wakati huu, wagombea waliokusudia kumpingania walilazimika kufanya kampeni za kumuunga mkono mtawala huyo. SOMA: Ulaya wahofia matumizi ya nyuklia

Kiongozi wa upinzani aliye uhamishoni, Svetlana Tikhanovskaya, alikosoa uchaguzi huu na kuuita kuwa ni kituko, huku Umoja wa Ulaya ukiutaja kuwa ni udanganyifu wa wazi.

Katika uchaguzi wa 2020, hali ya kisiasa ilikuwa tete baada ya wapinzani na mataifa ya Magharibi kudai kuwa Lukashenko alifanya udanganyifu mkubwa, huku mamlaka yakifanya msako mkali dhidi ya waandamanaji na wapinzani wa serikali.

Habari Zifananazo

Back to top button