ARUSHA: Katika kuadhimisha Siku ya Walimu Duniani 2024, Exim Bank Tanzania imechangia jumla ya mitungi ya gesi 1,000 kwa walimu mkoani Arusha ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika matumizi ya nishati safi.
Mchango huu ni sehemu ya jitihada za benki hiyo kuchangia ongezeko la matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuunga mkono kampeni ya kitaifa ya kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa kama vyanzo vya nishati.
Akizungumza wakati wa mkutano na walimu mkoani Arusha, Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa Exim Bank, Stanley Kafu, alisema benki hiyo imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha walimu wanakuwa katika mazingira safi na salama ili waweze kufanya kazi yao vizuri.

“Siku ya Walimu Duniani mwaka huu yeny4e kaulimbiu ya ‘Kuwezesha Wakufunzi: Kuongeza Utulivu, Kujenga Uendelevu’ inatupa fursa ya kutambua mchango mkubwa wa walimu kwenye jamii na katika elimu ya watoto wetu, amesema.
SOMA: “Ifikapo 2034 asilimia 80 watumie nishati safi”
Amesema taasisi hiyo ya kifedha imechukua hatua kwa lengo la kuwaondoa kwenye utegemezi wa kuni na mkaa.
Aliongeza kuwa matumizi ya nishati hiyo yatasaidia kupunguza gharama, muda, na kuchangia afya bora kwa walimu wetu,” alisema Stanley Kafu.
“Tunaamini kwamba mchango wetu unakwenda sambamba na azma ya Serikali ya kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
“Tunawapongeza walimu wa Arusha kwa kuwa mabalozi wa kampeni hii na kuchukua jukumu la kuhamasisha matumizi ya nishati safi katika jamii,” aliongeza Kafu.
Mchango huo ni sehemu ya mkakati wa Exim Bank kupitia programu yake ya ‘Exim Cares, ambayo inalenga kushirikiana na jamii katika miradi mbalimbali ya kijamii, ikiwa ni pamoja na elimu, afya, uwezeshaji na utunzaji wa mazingira.
Benki hiyo imejikita katika kuboresha ustawi wa jamii kupitia programu endelevu zinazolenga kuboresha maisha ya kila Mtanzania.