BFT kuibua vipaji vya mabondia wanawake

SHIRIKISHO la Ngumi Tanzania (BFT) limesema linatarajia kufanya shindano maalum mwishoni mwa mwezi huu ili kuibua vipaji vya mabondia wanawake watakaowakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa.

Akizungumza na SpotiLeo Rais wa BFT Lukelo Willilo amesema kutakuwa na mashindano ya kufuzu Kombe la Dunia hivyo, wanatarajia kufanya shindano la kutambua vipaji ambalo litafanya mchujo wa wale wenye uwezo.

Amesema anaamini kuna vipaji vingi ila havijapata nafasi ya kuonekana hivyo, huu ni wakati muafaka kwao kutumia fursa ya kuonekana.

Advertisement

“Tunao wanawake wachache kwenye mchezo huu, mpango wetu ni kuendelea kuwaibua na kuwapa nafasi ya kuonekana katika mashindano mbalimbali ikiwemo yajayo ya Kombe la Dunia,”amesema.

Amesema mipango ya kufanyika kwa mashindano hayo inaendelea na wanatarajia kupata ushiriki mkubwa wa vipaji vya wanawake.

Miongoni mwa timu ambazo zimekuwa zikiwapa nafasi wanawake katika michezo mbalimbali ni Jeshi na huenda wengi wakaonekana kutokea huko kwani wamekuwa na utamaduni wa kuibua vijana wengi na wanaofanya vizuri hutokea huko.

Mwisho